Matokeo ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Stand United yameiweka pabaya zaidi Ruvu Shooting na sasa huenda msimu ujao ikaaga Championship, huku benchi la ufundi likikiri ugumu.
Timu hiyo ya mjini Iringa juzi ikicheza kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ililazwa mabao 2-1 dhidi ya ‘Chama la Wana’ na kujikuta ikibaki mkiani ikiwa na pointi 11 baada ya michezo 26.
Kwa sasa maafande hao walioshuka daraja msimu uliopita wamebakiza michezo minne kumaliza msimu na iwapo watashinda yote watafikisha alama 23 ambazo hazitawaondoa kwenye mstari wa hatari.
Katika mechi zilizobaki za kuamua hatma ya timu, Shooting itacheza dhidi ya Pan African, Cosmopolitan na Green Warriors (ugenini) na Transit Camp itakayohitimisha nyumbani.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Julio Elieza alikiri hali kutokuwa shwari akisema wanasubiri lolote akieleza kuwa iwapo watafanikiwa kuangukia play off, huenda wakabaki kwenye ligi.
Alisema kwa sasa kinachohitajika ni nguvu ya pamoja ndani na nje ya uwanja kuhakikisha wanaungana kupata pointi 12 katika mechi zilizosalia ili kubaki kwenye ligi.
“Tunahitaji kukaza msuli sana katika mechi hizi zilizobaki ili kukwepa kushuka daraja moja kwa moja na tupate fursa ya kujitetea kupitia mechi za play-offs, kwa sasa tunahitaji nguvu ya pamoja kuhakikisha tunafikia malengo,” alisema kocha huyo.