Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruti za Simba, Yanga kimataifa

Simba X Yanga 1 Ruti za Simba, Yanga kimataifa

Sun, 15 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mara ya kwanza msimu huu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2023/24, itashuhudiwa miamba ya soka Bara, Simba na Yanga ikionyesha ubabe katika hatua ya makundi ambayo itaanza mwezi ujao kati ya Novemba 24–25 hadi Mechi 1–2 mwakani.

Siku chache zilizopita kule Afrika Kusini ilichezeshwa droo ambayo ilifanya kujua Simba na Yanga zimepangwa kwenye makundi gani katika mchakamchaka wa awamu ya 28 tangu michuano hiyo kutambulika kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa Simba huu ni mwendelezo miaka ya karibuni kuwa katika makundi ya Ligi ya Mabingwa, ila upande wa Wananchi ni baada ya zaidi ya miaka 20 iliyopita lakini cha kuvutia ni kwamba wamerejea wakiwa tishio kutokana na ubora wa kikosi chao kwa sasa.

Hiki ndicho kipindi ambacho mabosi wa klabu hizo pamoja na wadau hukuna vichwa kwani matumizi huongezeka na muda mwingine zaidi ya bajeti maana watatakiwa kusafiri katika mataifa mbalimbali kucheza michezo ya ugenini na hapo unaongelea gharama za usafiri zaidi ya watu 18, chakula, malazi na mengine.

BAJETI ZILIVYO

Kabla ya kuanza kwa msimu, Yanga ilikuwa ya kwanza kutangaza bajeti ambapo mkurugenzi wake wa Fedha, Sabri Sadick alitangaza Sh20.8 bilioni zitatumika msimu huu wa 2023/2024.

“Ndugu wajumbe pia tumeweza kutengeneza bajeti ya msimu ujao. Kutokana na mafanikio tuliyopata msimu huu (uliopita) kwa maana hiyo na msimu ujao tunatarajia kupata mafanikio zaidi na zaidi. Kwa hiyo katika makadirio yetu matumizi pekee ya bajeti yatafika mpaka bilioni 20.8 lakini vyanzo vya mapato bado tupo nyuma kidogo,” alisema Sabri.

Simba ilifuata kupitia kwa mtendaji mkuu, Imani Kajula ikitangaza bajeti ya Sh24 bilioni.

“Bajeti yetu ya mwaka 2023/2024 ni bilioni 23 nadhani mlisikia za wenzetu sitaki kulinganisha, mtakumbuka. Lakini kwa nini tunaamini kwamba ni muhimu tukuze mapato. Kuwa timu inayoongoza Afrika kunahitaji sana fedha. Kuongoza klabu kubwa ni gharama kubwa sana. Kwa hiyo mapato ni jambo la muhimu sana,” alisema Kajula.

MATUMIZI YA SAFARI

Gharama za makali ya safari za nje ziliwahi kumuibua makamu wa rais wa Yanga, Arafat Haji kwenye jukwaa la X-Space ambalo liliandaliwa na Mwananchi Communications Ltd (MCL) aliyeiomba serikali kuendelea kuwasapoti washiriki wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Arafat alisema safari moja inaweza kugharimu zaidi ya Sh230 milioni, hivyo ukipiga hesabu ya mechi tatu za hatua ya makundi ambazo ni ugenini unaongelea zaidi ya Sh600 milioni na kama timu inavuka hatua ya makundi ina maana kiwango hicho kinaweza kuongezeka.

“Ni timu chache Tanzania zinaweza kumudu hizo gharama (Simba, Yanga, Azam). Tunaomba Serikali izisaidie timu zingine ili ziweze kushiriki vizuri michuano ya kimataifa. Yanga tayari imekuwa chapa kubwa ya kuitangaza Tanzania, hivyo mpira ukipewa kipaumbele ni biashara kubwa,.” alisema.

UGUMU WA SAFARI

Ipo changamoto ya kutumia muda mrefu kwa safari ambayo kama kungekuwa na ndege nyingi au kutumia ndege maalumu unaweza kwenda na kurudi kwa muda mfupi. yote hiyo inatokana na uwepo wa ndege chache za kwenda katika baadhi ya nchi.

Imeshuhudiwa kwa misimu mingi namna ambavyo muda mwingine inabidi timu kusafiri kwa makundi huku zikitumia zaidi ya saa 18 kitu ambacho huondoa utulivu kuelekea mchezo husika.

Msimu uliopita Yanga ilikuwa na wakati mzuri kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Serikali ilitoa ndege hivyo ilikuwa rahisi kufika Algeria na kufanya vizuri kwenye mchezo huo ambao iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya USM Alger.

Lakini ilishindwa kutwaa ubingwa huo kutokana na kanuni ya bao la ugenini kwani mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani ilipoteza kwa mabao 2-1.

RUTI ZA SIMBA

Katika kundi B, Simba itakuwa na safari ya kwenda Botswana kati ya Desemba 1-2 kucheza dhidi Jwaneng Galaxy, Morocco kati ya Desemba 8-9 kucheza dhidi ya Wydad Casablanca na Ivory Coast kati ya Februari 23-24 mwakani kucheza dhidi ya timu ya zamani ya Azizi Ki na Pacoume, ASEC Mimosas.

Kutoka Tanzania hadi Botswana inaweza kuwa safari nyepesi kwa wekundu hao wa Msimbazi lakini safari ngumu itakuwa ya Morocco ambayo watakuwa na machaguo matatu la kwanza ni kupitia Uturuki, Dubai au Ethiopia na Ivory Coast njia nyepesi kwao ni kupitia Ethiopia.

YANGA NA MWEWE

Wananchi wanaonekana watakuwa na ruti mbili ngumu kwenye safari zao za kusaka nafasi ya kuvuka hatua ya makundi ya mashindano hayo ambazo ni Algeria kati ya Novemba 24-25 kwenda kucheza dhidi CR Belouizdad na kati ya Machi 1-2, mwakani ambapo itakuwa nchini Misri kucheza dhidi ya bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Al Ahly.

Safari hizo zinaweza kuwa na machaguo matatu kama itakavyokuwa kwa Simba kwenda Morocco kucheza dhidi ya Wydad Casablanca.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: