Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rui Pinto aibua hofu nzito Manchester City

Manchester City.jpeg Wachezaji wa Man City

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hofu kubwa imetanda katika ofisi za Manchester City baada ya mdukuzi wa masuala ya kimtandao Rui Pinto kuweka wazi kwamba anakaribia kuachia nyaraka za siri zinazoonyesha jinsi wababe hao wa EPL walivyokiuka sheria za matumizi ya pesa za FA ya England na Ulaya kwa ujumla.

Rui Pinto ambaye ni raia wa Ureno awali yeye ndio aliachilia nyaraka zilizoifanya Uefa ianzishe uchunguzi kisha ikaipa adhabu Man City juu ya makosa 115 ya ukiukaji wa sheria za matumizi ya fedha kwa makusudi.

Pinto, 35, ambaye alifichua nyaraka za kwanza mwaka 2018, anaeleza kwamba bado ana nyingine nyingi ambazo hajaziibua.

Taarifa za kifedha zilizovuja mwaka 2018, zilihusisha mkataba wa kocha wa zamani wa timu hii, Roberto Mancini, makubaliano ya haki za picha yanayomhusisha wakala wa Yaya Toure na barua pepe kuhusu mapato ya udhamini wa klabu.

Pinto anajiandaa kutoa nyaraka hizo muda wowote kuanzia sasa hali inayoweza kuiweka katika wakati mgumu Man City ambayo inatarajiwa kusikilizwa utetezi wake mwezi Novemba mwaka huu juu ya mashtaka 115 yanayoikabili.

Msimu uliopita miamba hii chini ya Pep Guardiola iliweka rekodi ya kushinda taji la nne mfululizo la Ligi Kuu England hali iliyowafanya kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo katika historia ya ligi hiyo.

Man City pia inadaiwa kufanya udanganyifu wa kifedha kwa kuingiza pesa kupitia vyanzo visivyo rasmi kisha kuzitumia katika shughuli za timu.

Inaelezwa wamekuwa wakionyesha wamesaini mikataba ya udhamini kwa pesa wakati wamesaini kwa pesa kiduchu tu bali pesa zilizozidi huwa ni zile wanazohitaji kuziingiza kwa njia ya udanganyifu.

Pinto, anaeleza kwamba kuna pesa ambazo Man City imezilipa katika maeneo mbalimbali ikiwemo na usajili lakini hazijaorodheshwa kwenye taarifa zao za mapato na matumizi walizotuma katika mamlaka za soka.

“Tutavujisha nyaraka, ingawa siwezi kusema lini lakini lazima nitafanya hivyo, nimepokea jumbe nyingi za vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana, najua hao ni mabosi wa timu za Ulaya na walikutana London kujadili kuhusu mimi ikiwa pamoja na taarifa zangu binafsi, wana wasiwasi sana juu ya nyaraka mpya ninazokwenda kuzifichua.” alisema Pinto.

“Nimefuatwa na baadhi ya maofisa wa Uefa wakitaka msaada juu ya uchunguzi wanaoufanya, ingawa sijawapa chochote lakini bado kuna nyaraka nyingi kuhusiana ukiukwaji wa sheria za kifedha uliofanywa na Man City.”

Awali, baada ya kuvujishwa kwa nyaraka na Uefa kufanya uchunguzi, iliifungia Man City kushiriki michuano ya Ulaya kwa miaka miwili na faini ya Pauni 25 milioni, lakini walikata rufaa na kushinda.

Pinto pia aliwahi kuvujisha mpango wa kuundwa kwa Europa Super League ulioanza kusukwa mwaka 2018.

Mamlaka za soka za England na Ulaya kwa ujumla zinazitaka timu zote kutumia pesa kulingana na mapato zinayoingiza, hili limeonekana kuwa jambo gumu kwa baadhi ya timu na muda mwingi huwa zinatumia zaidi ya mapato yao.

Ili kukwepa adhabu kwa kufanya hivyo, huwa zinaamua kuzidisha sifuri kwenye mapato kwa kuonyesha kwamba zimepata udhamini mkubwa ilhali sio kweli.

Adhabu kubwa inayoweza kuikumba Man City kwa makosa haya ya kukiuka sheria za matumizi ya pesa ni kushushwa Ligi Kuu, kufungiwa kusajili, kupokwa pointi ama kuwekewa kiwango cha matumizi ambacho hawatotakiwa kukivuka.

Chanzo: Mwanaspoti