Kocha Msaidizi wa AS Vita ya DR Congo, Roul Shungu ameeleza kuwa amepata nafasi ya kuongea na baadhi ya wachezaji wa Young Africans kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Young Africans itashuka katika Dimba la Royal Bafokeng uliopo kwenye mji wa Rustenburg, Afrika Kusini baadae leo Jumatano (Mei 17), ikiwa na lengo wa kuandika Historia ya kutinga kwa mara ya kwanza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Shungu ambaye aliwahi kufanya kazi Young Africans amesema amebahatika kuzungumza na Mshambuliaji Fiston Kalala Mayele na Kiungo Yannick Bangala na kuwataka kucheza kwa kujituma ili kuweza kuipeleka Fainali timu yao.
Shungu amesema: “Nimepata nafasi ya kuongea baadhi ya wachezaji akiwemo Mayele na Bangala kuelekea katika mchezo wao wa nusu fainali ambao naona nafasi kubwa kwao kuweza kuipeleka Yanga kucheza fainali kwa mara ya kwanza katika michuano hii mikubwa Afrika.
“Nimewaambia wanatakiwa kucheza kwa nidhamu kubwa bila ya kuangalia matokeo ya mchezo wa kwanza kwa sababu wapinzani wao wanapocheza kwao wamekuwa ni wagumu tofauti na wakiwa ugenini, wanatakiwa kujitahidi kupata bao la mapema ili kupunguza presha ingawa naamini wanaenda kucheza fainali,” amesema Shungu
Young Africans itaingia kwenye mchezo huo utakaoanza saa moja usiku kwa saa za Afrika Kusini, ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliopigwa juma lililopita jijini Dar es salaam.