Supastaa, Cristiano Ronaldo ameboresha rekodi zake za mabao baada ya kufunga mara nne katika mchezo mmoja akiwa na kikosi chake cha Al-Nassr.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 38 alifunga mara mbili kwenye kila kipindi dhidi ya Al-Wehda na kumfanya afikishe mabao 500 ya ligi kwenye maisha yake ya soka la kulipwa. Bao lake la kwanza kwenye mechi hiyo ya Al Wehda alifunga dakika 21 kwa shuti la chinichini lililompita kipa Abdulquddus Atiah.
Ronaldo alifunga bao la pili kwa kupitisha mpira kwenye uvungu wa miguu ya kipa huyo baada ya pasi ya kupenyeza na mapema baada ya kuanza kipindi cha pili, alifunga hat-trick yake ya kwanza akiwa na Al-Nassr. Bao la tatu alifunga kwa mkwaju wa penalti.
Bao la nne alifunga dakika chache baadaye akimalizia mpira uliopanguliwa na kipa baada ya shuti lake la kwanza. Lakini, mabao hayo wala hayakuwavutia mashabiki, ambapo walionekana kuelekeza lawama zao kwa kipa.
Shabiki mmoja aliandika kwenye Twitter: “Ona alivyoshangilia kwa nguvu kwa kufunga kwenye ligi ndogo kama kafunga fainali ya Kombe la Dunia.”
Shabiki mwingine aliandika: “Kipa kafanya ionekane kama ngumu vile.” Shabiki wa tatu aliandika: “Yule kipa kampa mabao mawili.”
Mashabiki wengine walishangaa Ronaldo kushangilia kwa nguvu kwenye ligi wanayoiona kuwa ndogo huku akifanya hivyo kwa staili yake ya “SIUUU”.
Mabao hayo manne yanamfanya Ronaldo kufikisha matano kwenye ligi tangu alipotua Al-Nassr akiwa amechezea timu hiyo mechi tatu.