Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ronaldo ataka kucheza Kombe la Dunia 2026

Ronaldo Num7 Ronaldo ataka kucheza Kombe la Dunia 2026

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

LISBON, URENO. KAMA ni njaa, basi ya Cristiano Ronaldo imezidi. Supastaa huyo wa Kireno kwenye kichwa chake anawaza rekodi tu.

Baada ya kuweka rekodi kibao kwenye soka, Ronaldo ameibuka na kusema anataka kuweka jina lake kwenye historia za kudumu, kuwa mwanasoka wa kwanza kucheza fainali sita za Kombe la Dunia.

Fowadi huyo aliyecheza klabu kadhaa kubwa za Ulaya ikiwamo Manchester United, Real Madrid na Juventus ameshaonyesha mafanikio makubwa kwenye soka la kimataifa, ambapo akiwa na Ureno alibeba ubingwa wa Euro 2016.

Ndiye kinara wa mabao kimataifa, akitikisa nyavu mara 115 katika mechi 182 alizochezea nchi yake.

Sa sa ripoti zinafichua anataka kujilinda kucheza kwa kiwango cha juu ili afike fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico.

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 36 kwa sasa anaonekana kuwa fiti huku akifurahia rekodi ya kutosumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Yaeye na mpinzani wake wa miaka yote Lionel Messi wanajiandaa kucheza fainali za tano za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani huko Qatar.

Wakifanikiwa hilo, wataingia kwenye orodha ya magwiji Lothar Matthaus wa Ujerumani na wakali wawili wa Mexico, Rafael Marquez na Antonio Carbajal waliocheza fainali tano tofauti za Kombe la Dunia.

Mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or, Ronaldo maarufu zaidi kama CR7 hana mpango wa kustaafu soka la kimataifa kwa kipindi cha karibuni, akitaka kuendelea kuitumikia Ureno zaidi na zaidi.

Ureno ina kila kitu na sasa inahitaji ushindi mmoja tu katika mechi nne zilizobaki ili kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika Qatar. Ronaldo atakuwa na miaka 41 kama ataendelea kucheza na kwenda kwenye fainali hizo za Kombe la 2026. Jambo hilo litaongeza idadi ya rekodi alizoweza staa huyo ambazo huenda zikachukua miaka mingi kuja kuvunjwa.

Tayari anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko mchezaji yeyote kwenye soka la kimataifa, huku akiweka rekodi nyingine kibao kwenye soka la klabu. Ronaldo, aliyewahi kucheza Sporting Lisbon hana mpango wa kustaafu kwa sasa na anaendelea kufanya mambo yake ndani ya uwanja.

Kwa sasa yupo Man United inayofanya hovyo kwenye ligi kiasi cha kutishia kibarua cha kocha wao, Ole Gunnar Solskjaer na alikuwamo uwanjani wakati miamba hiyo ya Old Trafford ilipochapwa 5-0 na Liverpool.

Wakati huo huo, Ronaldo juzi Alhamisi alitangaza kuwa mpenzi wake mrembo Georgina Rodriguez anatarajia kujifungua pacha ambao watamfanya kuwa na jumla ya watoto sita.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz