Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amesisitiza sasa analala usingizi mnono baada ya Cristiano Ronaldo kuondoka na kujiunga na Al-nassr kutoka Saudi Arabia.
Ten Hag akaendelea akidai heshima imerudi ndani ya klabu hiyo baada ya Ronaldo kuondoka kufuatia mahojiano yake aliyofanya na mtangazaji maarufu Piers Morganl.
Katika mahojiano hayo Ronaldo aliwaponda mabosi wake akiwemo Ten Hag akisema hamuheshimu kocha huyo kwasababu hakuonyesha heshima kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari Ten Hag alisema; "Siku za nyuma kulikuwa na mambo ya hovyo, sina sababu ya kudanganya, wachezaji wakubwa hata kama nje ya uwanja sheria lazima ifuate mkondo wake, kila taasisi ina sheria zake, kama sheria haitafuatwa mambo hayatenda vizuri, nilikua nahofia usingizi wangu lakini sasa nalala usingizi mnono, natakiwa kutoa maamuzi kwa heshima ya klabu na manufaa kwa kila mtu," alisema Ten Hag.
Tangu Ten Hag alipotua Old Trafford heshima imerudi ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji, vile vile wachezaji wake wameonyesha ushirikiano mzuri ndani na nje ya uwanja.
Mholanzi huyo akakiri kwa mara nyingine "Nilikua na sababu kwasababu nilihofia tatizo linaweza kutokea, maamuzi yangu pia yanaangalia matokeo ya jambo husika, lakini sasa sina mashaka kabisa,"
Tangu Ronaldo alipoondoka Man United imebadilika na imeendelea kufanya vizuri katika mashindano yote kama Kombe la FA, na Ligi ya Europa.
Chini ya kocha huyo Man United imebeba taji lake la kwanza msimu huu (Kombe la Carabao) kwenye fainali iliyochezwa uwanja wa Wembley dhidi ya Newcastle wiki moja iliyopita.
Hadi tunaelekea mitamboni Man United ilikuwa dimbani ikimenyana na Liverpool kwenye mchezo wa ligi uwanja wa Anfield.