Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ronaldo? Hazard anatafuta kiki mjini

Hazard X Ronaldo Ronaldo? Hazard anatafuta kiki mjini

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mdahalo wa nani zaidi, Cristiano Ronaldo na Lionel Messi umechukua sura mpya.

Kumpata mshindi ni shughuli pevu. Vita yao ni kali. Mmoja amebeba Ballon d’Or tano, mwingine amenyakua nane. Wote wawili wamebeba Ballon d’Or 13, si mchezo.

Kwa pamoja wameshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tisa, Messi nne, Ronaldo tano na mataji mengine kibao ya ligi. Messi amejiongeza, ameshinda taji la Kombe la Dunia 2022, Ronaldo amebeba Euro 2016.

Lakini, sasa supastaa, Eden Hazard ameibuka na kuchochea moto. Mbelgiji huyo amedai Messi ndiye mwanasoka bora zaidi kuwahi kutokea duniani na hakujali hilo linamtofautisha na Los Blancos, kwa kumuweka kando Ronaldo. Ronaldo na Hazard wote ni wachezaji wa zamani wa Real Madrid.

Kwenye umri wa miaka 33 tu, Hazard tayari ameshastaafu, alitundika daruga zake Oktoba mwaka jana.

Lakini, Ronaldo, jana Jumatatu alitimiza umri wa miaka 39 na bado anakipiga. Messi, 36 bado anakipiga.

Hazard alikuwa na misimu saba mitamu Chelsea alikojiunga akitokea Lille mwaka 2012. Kisha alihamia Real Madrid, ambako maisha hayakuwa matamu kabisa. Miaka yake minne ilikuwa ya mateso ya kupata majeraha ya mara kwa mara hadi hapo alipoona inatosha, akatundika daruga zake.

Akizungumza na gazeti la Ufaransa la L’Equipe, Hazard alisema kuhusu mchezaji ambaye anadhani alikuwa bora kumzidi - na hakumtaja Ronaldo.

Hazard alisema: “Binafsi, Messi ni yeye tu. Nilikuwa napenda kumtazama, ni mchezaji bora wa kihistoria. Ngumu sana kuchukua mpira kutoka kwake. Cristiano ni mchezaji mkubwa kunizidi, lakini kwenye upande wa soka halisi, sidhani. Labda, Neymar.

“Ni hivyo, sio bora kunizidi. Pale Real Madrid mtu unakuwa bora, watazame (Karim) Benzema, (Luka) Modric wote walikuwa bora, (Toni) Kroos, Kev (De Bruyne) nao wanasoka lao la kipekee.”

Messi na Ronaldo wamecheza mechi nyingi, wamefunga mabao mengi na wameasisti mara nyingi kumzidi Hazard. Messi amefunga mabao 821 katika mechi 1,033 alizocheza kwenye klabu na timu ya taifa, wakati huo akiasisti mara 400. Ronaldo amefunga mabao 867 katika mechi 1,198 - ikiwamo mabao 450 katika mechi 438 alizocheza Real Madrid. Mreno huyo ameasisti mara 282.

Kwa upande wake, Hazard amefunga mabao 200, ameasisti 193 katika mechi 748 alizocheza maishani mwake.

Aliibeba Lille kunyakua Ligue 1 na Kombe la Ufaransa, kisha alibeba Ligi Kuu England mara mbili, Kombe la FA, Kombe la Ligi mara mbili na Europa League mara mbili akiwa na Chelsea.

Huko Real Madrid aliishia kufunga mabao saba tu katika mechi 76, lakini alishinda ubingwa wa La Liga mara mbili na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja. Kwa takwimu za mastaa hao, ni wazi kabisa Hazard anatafuta kiki.

Chanzo: Mwanaspoti