Mfungaji wa bao pekee na la ushindi wa Manchester City, Rodri amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wa msimu na Shirikisho la soka Ulaya, UEFA.
Wachezaji saba wa Man City wametajwa kwenye timu bora ya msimu na Erling Haaland akitwaa tuzo ya bao bora la msimu.
Bao la Rodri dakika ya 68 lilifanya tofauti wakati City ilipoilaza Inter Milan 1-0 mjini Istanbul nchini Uturuki Jumamosi na kubeba Kombe la Ulaya na kukamilisha msimu kwa mataji matatu.
Na Jumapili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alitawazwa mchezaji bora wa msimu na jopo la waangalizi wa kiufundi la UEFA.
Rodri alicheza katika mechi zote isipokuwa moja ya Ligi ya Mabingwa ya City msimu huu, huku Jumamosi (Juni 10) akifunga bao lake la pili katika mashindano hayo.
Kiungo huyo wa kati wa Hispania alijumuishwa na wachezaji wenzake sita katika timu ya msimu huu ambao ni Haaland, Kevin De Bruyne, John Stones, Ruben Dias, Bernardo Silva na Kyle Walker.
Federico Dimarco wa Inter na Alessandro Bastoni pia walichaguliwa pamoja na kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois na fowadi Vinicius Junior.
City pia ilinyakua tuzo ya bao bora la msimu kupitia kwa Haaland kwa bao lake la sarakasi dhidi ya klabu ya zamani ya Borussia Dortmund wakati wa hatua ya makundi, alipopinda na kugeuza pasi ya Joao Cancelo na kutinga wavuni wakati City iliposhinda 2-1.