Kocha Mkuu wa Simba Sc, Roberto Oliveira ‘Robertino’ amewapongeza wachezaji wake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC.
Simba SC ilipata ushindi huo Jumamosi (Oktoba 28) katika mchezo wake wa sita wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Washambuliaji Jean Baleke kutoka DR Congo na Moses Phiri wa Zambia kila mmoja alifunga bao moja na kuipa ushindi timu hiyo, wakati bao la lhefu likifungwa na Ismail Mgunda.
Akizungumza jijini Dar es salaam Robertinho amesema wachezaji wake walijituma kwa kiasi kikubwa na kusaidia timu hiyo kuvuna alama tatu.
Kocha huyo kutoka nchini Brazili huyo amesema wapinzani wake waliingia na mbinu bora, lakini haikuwazuia wachezaji wake kuonyesha kiwango kikubwa kutimiza lengo la kushinda mchezo huo.
“Nawapongeza wachezaji wangu, haikuwa kazi rahisi lakini kikubwa tumepata alama tatu muhimu nyumbani,” amesema.
Pia, kocha huyo amesema waliingia katika mchezo huo wakiwa hawajapata muda wa kutosha kujiandaa baada ya kutoka nchini Misri kucheza mechi ya marudiano ya Robo Fainali ya African Football League dhidi ya AI Ahly.
“Ratiba imekuwa ngumu kwetu, tumetoka kushiriki michuano mikubwa ya African Football League (AFL), tulifanya mazoezi siku mbili kabla ya mchezo (dhidi ya Ihefu),” amesema.
Kocha huyo amesema baada ya kuifunga Ihefu FC, hivi sasa anaelekeza akili yake katika mchezo ujao wa ligi hiyo dhidi ya Young Africans utakaopigwa Jumapili (Novemba 05).
Simba SC inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 18 sawa na kinara Young Africans, zikitofautiana idadi ya mechi pamoja na mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba SC imecheza mechi sita ikishinda zote, huku Young Africans ikicheza mechi saba, ikishinda sita na kufungwa mchezo mmoja.