Ngomaa ni nzito leo kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira raia wa Brazil kuikabili Dodoma Jiji bila uwepo wa mashine sita za kikosi cha kwanza, ukiwa ni mtego kwake.
Huu unakuwa ni mchezo wa pili kwa kocha huyo maarufu Robertinho baada ya ule wa kwanza alipopewa mikoba ya Zoran Maki, ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 3-2 Mbeya City.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, ameliambia Spoti Xtra kuwa: “Tunahitaji pointi tatu, lakini kuna baadhi ya wachezaji tutawakosa kama Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute, Joash Onyango, kuwakosa hawa wakati huu unakuwa na mechi ngumu kwelikweli.
“Waliopo wana kazi ya kuonesha kuwa kwa nini wapo ndani ya kikosi cha Simba, hivyo mashabiki wa Simba mjitokeze kwa wingi Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.”
Mbali na nyota hao, pia mshambuliaji Moses Phiri mwenye mabao 10, Henock Inonga mwenye mabao mawili pamoja na Peter Banda mwenye bao moja, hawatakuwa kwenye mchezo wa leo.
Sababu kubwa ya nyota hawa kuukosa mchezo wa leo dhidi ya Dodoma Jiji ni kutokuwa fiti baada ya kupata maumivu kwenye mechi zilizopita.
Phiri aliumia kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambapo ubao wa Uwanja wa Kaitaba ulisoma Kagera Sugar 1-1 Simba, Banda alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Singida Big Star Uwanja wa Liti, ubao ulisoma Singida Big Stars 1-1 Simba na ni Banda alitupia bao.
Inonga alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Simba 7-1 Prisons.