Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho kurudisha kampa, kampa tena SC

Robertinho X Ushindi Kocha wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’

Sat, 11 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesikia kilio cha mashabiki wa klabu hiyo wanaotaka shoo shoo uwanjani wakati timu hiyo ikipata ushindi kwa kuwaambia; ‘Subirini sasa boli litatembea’.

Kauli ya kocha huyo ambaye hana muda mrefu tangu alambe ajira hiyo kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Zoran Maki’, imekuja saa chache tangu kikosi cha Simba kitoke kutoa dozi ya pili mfululizo kwa Vipers ya Uganda, huku wakiweka hai matumaini ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Robertinho anaamini kwa hatua waliyopo walihitaji ushindi zaidi, ili kuwa kwenye mwelekeo mzuri na suala la kandanda la kuvutia litakuja taratibu kwenye kikosi chake kwani mpango wake ni kujenga timu inayocheza soka safi la kuvutia.

Kocha huyo alisema ni vizuri mashabiki kuendelea kumuunga mkono maana nafasi yao kwenye timu ni kubwa, huku mengine akiwataka wamwachie yeye kwani kila kitu kitakuwa sawa.

“Ulikuwa ushindi muhimu ambao tulikuwa tukiuhitaji, tulijua kuwa mchezo ni lazima ungekuwa mgumu lakini jambo zuri kwetu ni kwamba tulipata ambacho tulihitaji. Ni kazi yetu makocha kuhakikisha tunaimarisha timu kwenye kila eneo lakini wakati huo mchakato ukiendelea yanatakiwa kupatikana matokeo mazuri,” alisema Robertinho.

Alisema malengo yake ni kuifanya Simba kuwa tishio Afrika na sio Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki pekee hilo haliwezi kuwa kwa siku moja, na ni jambo ambalo linawezekana kama kila mmoja akiamini na kuweka mawazo yao pamoja.

“Japo mambo ambayo tunafanya hatua kwa hatua, kwa sasa mpango wetu ni kuhakikisha kunafanya vizuri dhidi ya Horoya lakini hatuwezi kuwa na mawazo yetu yote huko kwa sababu tutakuwa na mchezo wa ligi ambao nao tunatakiwa kushinda,” alisema.

Kabla ya kuivaa Horoya kuwania kufuzu robo fainali, itacheza leo dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Ligi, huko Manungu. Simba ilitinga hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni msimu wa 2018–19 na 2020–21. 2003 ilitinga nane bora kwenye michuano hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live