Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’, amesema atafanya mabadiliko makubwa ya kiufundi pamoja na kupanga mikakati mipya kutokana na mbinu za wapinzani wao, Horoya AC kutoka nchini Ghana.
Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kesho Jumamosi (Machi 18), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia saa moja usiku.
Kocha Robertinho amesema kuwa, wana kazi kubwa kwenye mchezo huo kwa sababu mashindano hayo siyo mepesi lakini wanahitaji matokeo mazuri.
“Tunapaswa kuwabadilishia mipango kulingana na namna ambavyo tutakutana nao hasa kwenye sehemu ya mazoezi hapo ndipo tunafanyia kazi makosa yetu. Wachezaji ambao tunao wengi wana vipaji na wanapambana kutafuta matokeo na hakuna ambaye hatambuí ubora wa wapinzani wetu.”
“Tulipoteza dhidi yao kutokana na wao kutumia makosa yetu na kufanikiwa kufunga bao 1-0, ninaimani hayawezi kujirudia baada ya kuweka mpango mkakati wetu vizuri kupata ushindi na kucheza robo fainali,” amesema Robertinho.
Simba SC ipo nafasi ya pili katika msimamo Kundi C ikiwa na alama 06 wakati vinara wa kundi hilo Raja Casablanca ya Morocco wakiwa na alama 12 baada ya kucheza michezo minne.
Horoya AC ya Guinea ipo nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 04, huku Vipers SC ikiburuza mkia kwa kuwa na alama 01.