Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewakalia kooni wachezaji wake akiwaambia wakati wanajiandaa kucheza na Coastal Union akili zao ziwaze kulinda heshima kwa kuhakikisha Wekundu hao wanatinga kibabe makundi ya CAF.
Robertinho amesema baada ya kikao chake na wachezaji kuna mkataba muhimu wamekubaliana wataingia na akili kubwa kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Power Dynamos wakiwa na lengo moja tu kuthibitisha ubora.
Alisema wamekubaliana kwamba makosa yaliyozalisha sare ya mabao 2-2 ugenini, Ndola nchini Zambia hayakuwa ya mtu mmoja au wawili na kwamba timu nzima ilikosea, lakini dakika 90 za nyumbani zitakuwa na mabadiliko makubwa. Simba itarudiana na Dynamos, Oktoba Mosi ambapo Wekundu wanahitaji suluhu, sare ya bao 1-1 au ushindi wowote kutinga hatua ya makundi.
“Tumezungumza na wachezaji tulichokubaliana matokeo yaliyopita yametufunza kitu. Hapa hatuzungumzii makosa ya mtu mmoja au wawili tunapoteza kama timu, tunadroo kama timu na tunashinda kama timu. Sasa akili kubwa ni kuangalia mambo yanayotukabili mbele,” alisema Robertinho.
“Ninachowaambia mashabiki wetu waje uwanjani siku ya mchezo. Simba sio timu ya kuishia hapa tumekubaliana na wachezaji wangu kwamba tunatakiwa kushinda hapa, na tutafanya hivyo.
“Tunahitaji kila mchezaji kuamka. Hii ni klabu kubwa mashabiki hawataki kuona tunapata matokeo ambayo hayawafurahishi. Nina imani watafanya makubwa kwa kuwa na wao wameumia na ile sare.”
AKILI ZOTE COASTAL
Robertinho alisema watautumia mchezo wa leo Alhamisi dhidi ya Coastal Union kama dakika 90 muhimu za kujiandaa kisaikolojia ili kushinda mchezo wa marudiano dhidi ya Dynamos.
“Tunajua mabadiliko ya Coastal Union haitakuwa mechi rahisi, lakini kitu muhimu ni kushinda kuanzia mechi hii. Tunatakiwa kuonyesha ukubwa wetu ili watu wajue tulikosea kule na hapa tutarekebisha,” alisema.