Simba imefanya usajili mkubwa kwa ajili ya msimu huu wa mashindano. Imeshusha vifaa vya maana kwelikweli.
Imewashusha Che Fondoh Marlone, Leandre Onana, Luis Miquissone, Aubin Kramo na wengineo. Kwa kifupi Simba imefanya kazi yake kwenye usajili vyema sana.
Ni wazi kuwa wana matarajio makubwa na usajili wao. Kila eneo wamelifanyia maboresho kuanzia kwenye ulinzi hadi ushambuliaji. Wangefanya nini zaidi ya hiki? Hakuna.
Hata hivyo kuna sababu tatu kubwa za Simba kufanya usajili wa aina hii.
Sababu ya kwanza ni kurejesha heshima yake kwenye mashindano ya ndani. Kwa miaka miwili sasa Simba haijashinda taji lolote la ndani. Ni fedheha kubwa sana kwao.
Ubaya ni kwamba wakati Simba ikiambulia patupu, mataji hayo yamekwenda kwa watani zao Yanga. Inaumiza sana kwa Wanasimba.
Viongozi wa Simba wanaamini kuwa wamempa kila kitu ambacho anastahili kuwa nacho ili kushinda mataji msimu huu.
Juzi hawakufurahishwa sana na namna timu yao ilivyocheza dhidi ya Singida Fountain Gate. Wanatazamia kuona mabadiliko makubwa hii leo.
Pili Simba inataka kushinda taji la Ligi Kuu msimu huu. Wamelikosa mara mbili mfululizo. Mashabiki wa Simba hawataki unyonge huu tena. Wataweza? Ni suala la kusubiri na kuona.
Pia wanataka kushinda taji la FA. Kwa miaka miwili mfululizo pia wameshindwa kupata taji hilo.
Mwaka juzi walifungwa na Yanga kwenye nusu fainali pale Mwanza. Mwaka jana wakatolewa pia kwenye hatua hiyo pale Mtwara na Azam FC. Inawaumiza sana.
Mwaka huu wanahitaji pia kushinda taji hilo. Wanaamini kuwa wana timu bora zaidi ya Yanga, zaidi ya Azam FC. Wataweza kufanya hivyo?
Sababu ya pili kubwa kwa Simba kufanya usajili wa maana ni kufikia malengo yao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Wanataka kufika nusu fainali.
Kila mwaka wamekuwa wakiweka wazi kuwa lengo lao ni kufika hatua hiyo.
Mwaka jana waliishia hatua ya robo fainali. Waliondoshwa na Wydad Casablanca kwa mikwaju ya penalti. Kwa kifupi ni kwamba walikaribia kabisa malengo yao.
Hata hivyo walifika hatua hiyo wakiwa na timu ya kawaida. Msimu huu wameiboresha zaidi. Wameipa nguvu zaidi.
Huu ni mtihani mkubwa zaidi kwa Robertinho. Simba wanasubiri awafikishe nchi ya ahadi. Kama ni robo fainali wameshazoea. Kwa sasa wanataka zaidi.
Sababu kubwa ya tatu ya usajili wa mwaka huu ni kufanya vizuri kwenye mashindano ya Super League (African Football League). Ni mashindano ya vigogo wanane wakubwa Afrika.
Simba ndio wawakilishi pekee wa Afrika Mashariki. Na ufunguzi wa mashindano haya utafanyika Tanzania. Ni heshima kubwa kwa Simba ila kwao ni lazima wafanye vizuri.
Huku kuna kina Al Ahly, Wydad, Mamelodi, Esperance na wakubwa wengine wa Afrika. Simba imefanya usajili mkubwa kwa sababu hii.
Mwisho wa siku huu ndio mtego mkubwa kwa kocha wao. Lazima aamue kusuka au kunyoa.
Anatakiwa kuhakikisha nyota wapya wanaingia kwenye mfumo kabla ya kazi hii kubwa. Watu wanataka kuwaona kina Miquissone, Kramo na wengineo wakiuwasha moto.
Ubaya ni kwamba kwa Robertinho bado ameendelea kuwaamini wachezaji walewale waliokuwepo. Hawa kina Kibu Denis na wengineo. Kuna muda mashabiki watataka kuona zaidi. Itabidi awe ameshaamua moja. Kusuka au kunyoa.