Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema baada ya kumaliza michezo ya Hatau ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kurejea nchini Tanzania, sasa nguvu zao wanazielekeza katika michezo mitatu ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans.
Simba imerejea nchini jana Jumapili (April 02) kutokea Morocco kwenye mchezo wao wa kukamilisha hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablaca ambayo ilishinda 3-1, lakini hata hivyo, timu hizo zote zilishafuzu Robo Fainali katika Kundi lao la C.
Robertinho, amesema michezo michezo ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea mchezo wao wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo mpinzani wao watamjua keshokutwa, Jumatano (April 05).
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema michezo hiyo mitatu ikiwamo michezo miwili dhidi ya Ihefu FC mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans ataitumia kwa ajili ya kujiandaa na michezo yao miwili ya Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Amesema wachezaji wake hawakucheza vibaya kwenye mchezo uliopita dhidi ya Raja Casablanca na kwamba walicheza vizuri na kuonesha kiwango kizuri, licha ya kufungwa.
“Nimefurahi kuona Simba SC imefuzu kucheza hatua ya Robo Fainali licha ya kupoteza mchezo dhidi ya Raja Casablanca, sasa akili na nguvu tunazielekeza kwenye michezo iliyopo mbele yetu ikiwa ni pamoja na kushinda dhidi ya Young Africans na kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.”
“Kuhusu wachezaji wangu wawili Mohammed Hussein (Tshabalala) na Sadio Kanoute ambao hawakuwapo katika mchezo uliopita, sasa nitaungana nao kuelekea michezo yetu ijazo kuhakikisha tunafikia malengo,” amesema Robertinho
Simba SC itacheza Robo Fainali ya ASFC dhidi ya Ihefu FC Ijumaa (April 07) katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, kisha itacheza tena dhidi ya timu hiyo ya mkoani Mbeya katika mchezo wa Ligi Kuu April 10, na siku sita baadae itakutana na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.