Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho awaachia msala Uongozi Simba SC

Robertinho X Bocco Robertinho awaachia msala Uongozi Simba SC

Sat, 3 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imeendelea kujifua katika uwanja wake wa Mo Simba Arena, Bunju na wakati huohuo wakiweka mipango ya msimu ujao ikiwemo usajili unaoendelea kimya kimya huku mastaa wake wakiwekwa kiporo.

Wanamsimbazi hao ni kama wamemaliza hesabu za msimu huu kiaina licha ya kubakiza mechi mbili za ligi dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union, kwani akili yao kubwa ipo kwenye msimu ujao ambapo vikao vya mara kwa mara vinaendelea ili kuhakikisha wanarudi kwenye ufalme wao walioupoteza kwa misimu miwili ukienda kwa watani zao Yanga.

Ili kuhakikisha hilo, Kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira Robertinho amewaambia viongozi kumalizana haraka na mastaa waliopo kikosini ndani ya siku tisa kabla Ligi haijamalizika ili baada ya mechi mbili za mwisho awape mapumziko kabla ya kuanza msimu mpya.

Robertinho tayari ametoa ripoti kwa uongozi ya wachezaji anaotaka kusalia nao kikosini, na amewaeleza vigogo wa timu hiyo kama kuna mtu mwenye shida au changamoto ya kimkataba basi wamalizane mapema ili akapate muda wa kutosha kupumzika kabla ya kurudi kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya 'Pre Season' inayotarajiwa kuwa nje ya nchi.

Hadi sasa ni Saidi Nitbanzokiza 'Saido', pekee aliyepewa ruhusa ya kwenda kwao Burundi kwa mapumziko na wengine watapewa mapumziko kuanzia tarehe 10 mwezi huu huku wengine wakiwemo Gadiel Michael, Nelson Okwa, Agustine Okrah, Ismail Sawadogo na Mohammed Ouattara wakitarajiwa kuachwa jumla.

"Kocha anataka wachezaji waliotumika sana msimu huu wapate muda wa kutosha kupumzika, kuna majina ameyapendekeza kubaki kikosini na wapo ambao amesema waondoke, hivyo tunafanya utaratibu wa kumalizana nao kwenye mambo ya kimkataba na malipo kisha tuwape mapumziko na wengi wataondoka baada tu ya msimu kuisha.

Watapumzika kwa muda wa siku 20 hadi mwezi, baada ya hapo watarudi kambini kwa maandalizi ya 'Pre Season' tunayopanga kwenda nje, kocha anataka aanze mapema maandalizi ya msimu ujao akiwa na kikosi kamili kwa maana ya watakaobaki na watakaosajiliwa," kilieleza chanzo chetu.

AKILI KUBWA

Katika nafasi nyingine Simba imeshtukia kitu kwenye usajili na haraka imetumia akili kubwa kutatua jambo hilo na kuweka mipango ya namna litaenda.

Awali Simba kulikuwa na mvutano wa chini chini kuhusu usajili ambapo baadhi ya viongozi walikuwa na majina yao na kocha alikuwa na majina yake jambo ambalo kwa pamoja wameona litaigharimu timu na kuamua waungane kwenye usajili.

Mwanaspoti limepenyezewa, baada ya vuguvugu hilo, uongozi umeamua kumpa majina yote kocha kwa maana ya yale waliyoyapendekeza viongozi mbalimbali wa klabu na yale ya kocha mwenyewe kisha aamue nani anamtaka na baada ya hapo wataangalia uwezekanao wa kumpata kwa kuzingatia bajeti yake na matakwa mengine.

Tayari kocha amewapitisha beki na nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya Rwanda, Thierry Manzi sambamba na winga Mcameroon, Leandre Onana na sasa anawatazama wachezaji wengine waliopendekezwa na uongozi na mwisho wa siku ataamua asajiliwe nani.

"Kuna kitu tumekishtukia, awali kila kiongozi alitaka alete mchezaji wake, hii tumeona itatuvuruga na jukumu hilo sasa tumemuachia kocha.

Hatujakataa viongozi kupendekeza wachezaji lakini jukumu la mwisho litabaki kwa kocha kuwapitisha au kuachana nao, hatutaki kumuingilia na tutamsapoti kwa kila jambo kadri tutakavyoweza." kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya Simba.

Miongoni mwa wachezaji ambao majina yao yapo mezani kwa Simba ni viungo Sospeter Bajana wa Azam, Bruno Gomes wa Singida Big Stars, winga Kramo Aubin na beki Coulibaly Wanlo kutoka Asec Mimosas sambamba na Manzi na Onana walio Rwanda kwa sasa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: