Kocha Mkuu wa Simba Roberto Oliveria amewaambia wachezaji anataka mpira uchezwe zaidi kwenye eneo la wapinzani wao na si kwao, huku akianzisha mazoezi maalum kwa ajili ya wanaocheza katika safu ya mbele tu.
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Saido Ntibazonkiza, alisema hayo katika mahojiano maalum jijini, Abu Dhabu, Falme za Kiarabu walikoweka kambi ya muda mfupi.
Ntibazonkiza aliyesajiliwa na Simba kipindi hiki cha dirisha dogo, alisema Robertinho ameegemea zaidi katika eneo la ushambuliaji na hata baada ya mazoezi ya timu nzima, bado anakuwa tena na programu maalum ya ziada kwa ajili ya kufundisha namna ya kushambulia ambayo anawapata mastraika, mawinga na viungo washambuliaji.
"Mazoezi yanakwenda vizuri na wachezaji tupo vizuri majeruhi wameshaanza kurejea, kweli kocha mkuu kuna kitu amekibadilisha, kwa wachezaji tunafurahia mazoezi na kuna kitu anachotuongezea, hasa upande wa ushambuliaji tunaona kuna kitu kikubwa anatupa," alisema mchezaji huyo raia ya Burundi.
Alisema kwa aina ya mazoezi wanayofanya, ana imani siku zinavyozidi kusonga mbele, eneo la ushambuliaji la timu yao litakuwa limebadilika kwa kiasi kikubwa.
"Alivyofika tu na kuanza mazoezi, alituambia tuchezee sana upande wa mpinzani, ndiyo maana amekuwa akitukomalia sana sehemu ya mbele na hata baada ya mazoezi huwa na mazoezi mengine maalum kwa wachezaji wanaocheza nafasi ya mbele, ametusaidia na tukiendelea hivi naona mstari wa mbele utakuwa hatari sana," alisema Ntibazonkiza.
Nyota huyo pia alionyesha kufurahishwa jinsi alivyopokewa na wanachama na mashabiki wa timu hiyo, huku akimpongeza shabiki mmoja aliyeweka picha yake kubwa kwenye bajaji na kuandika 'kumbe siyo mzee.'
Picha ya bajaj hiyo ameonekana kuvutia wengi kwenye mitandao ya kijamii, huku mwenyewe akisema ameiona.
"Nimeiona ile bajaj, nilicheka sana, na bado Mwenyezi Mungu ndiyo hakimu. Sikutarajiwa vile ila nashukuru kuona kuna mashabiki wananisapoti, wananikumbali, naomba wanachama na mashabiki wa Simba wazidi kunisapoti, watarajie mazuri zaidi yanakuja," alisema nyota huyo.
Wakati huo huo, Simba imepangwa kukutana na Coastal Union katika mechi ya Kombe la FA wakati Azam FC ikitarajiwa kuwavaa Dodoma Jiji kati ya Machi 3 hadi 5, mwaka huu hapa jijini.
Kwa mujibu wa droo iliyochezeshwa jana, Namungo itaicheza dhidi ya Ihefu, Kagera Sugar wataikaribisha Ken Gold, Mtibwa Sugar watawavaa Buhaya FC, Geita Gold itacheza dhidi ya Nzega United huku Gwambina itakuwa nyumbani dhidi ya Pan African.
Mashujaa wao watacheza dhidi ya Prisons na kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya kutakuwa na 'dabi' kati ya Mbeya Kwanza dhidi ya Mbeya City wakati KMC itawaalika Copco, Polisi Tanzania vs JKT Tanzania, Mapinduzi vs Polisi Katavi, Green Warriors vs Mbuni na New Dunde itawaalika African Sports.