Kocha wa Simba Robertinho, Oliveira ameshauriwa kutumia kikosi kilichocheza dakika 45 za pili, katika mchezo wa marudiano dhidi ya Power Dynamos.
Simba iliambulia sare ya mabao 2-2 kwa mbinde kwenye mchezo wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika matokeo yaliyowasononesha mashabiki wao hasa baada ya Yanga kushinda 2-0, ugenini dhidi ya Al Merrikh ya Sudan.
Kocha Choki Abed alisema, wachezaji walioanza kipindi cha kwanza walishindwa kuchangamka kama ambavyo walioingia kipindi cha pili.
Alisema baada ya kufanya mabadiliko kuingia Fabrice Ngoma, Luis Miquissons, Saido Ntibazonkiza na Jean Baleke, John Bocco mchezo ulibadilika sana.
“Kocha namshauri ajitahidi walioingia kipindi cha pili ndio watakaomwokoa katika mchezo wa marudiano maana baada ya wao kuingia mchezo ulibadilika sana.
“Baleke alikosa umakini lakini ndio mpira ulivyokuwa kama angetulia wangepata matokeo zaidi ya hayo naamini mwalimu mwenzangu ameliona hilo na atalifanyia kazi,” alisema Abeid.
Naye mchezaji wa zamani wa Simba, Monja Liseki alisema kilichoikosesha Simba matokeo ni kukosa umakini kwa safu ya ushambuliaji ambayo ilikosa kujiamini.
Alisema wanatakiwa kubadilika na kujiamini katika eneo la kufunga kwani wangetulia wangepata matokeo mazuri zaidi.