Simba SC imeondoka juzi asubuhi kwenda Zambia, kuwahi pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akionyesha vidole vitatu bila na kutoa ufafanuzi, lakini mastaa wa timu hiyo wakisema wanaenda kuweka heshima ugenini.
Kikosi hicho kiliondoka saa 5 asubuhi na Kocha Robertinho akizungumza na Mwanaspoti kabla ya kupanda ndege kwenda Ndola ambapo watacheza mechi hiyo ya Caf kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, alisema wanaenda kufanya mambo makubwa matatu yatakayowabeba kwenye mechi hiyo.
Kocha Robertinho alisema wanawaheshimu wapinzani wao, lakini wanaenda timu haitakuwa ikikaba na badala yake itashambulia mwanzo mwisho ila watacheza kwa ubora wa hali ya juu na kuzuia nafasi zote ili kupata matokeo mazuri ugenini kabla ya mechi ya marudiano wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo atatinga makundi na itakayopigwa itaacha rasmi michuano hiyo kwa msimu huu kwani ile ofa ya kucheza play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika safari hii imefutwa na CAF.
“Sio mchezo mwepesi ila naamini kwenye maeneo matatu kuzuia, kukaba na kushambulia hiyo ni mbinu nitakayoitumia katika mchezo huo wa Jumamosi,”amesema Robertinho akifafanua mambo hayo atakayoenda nayo kwenye mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa raundi hiyo ya pili ya Ligi ya Mabingwa.
“Mashabiki wameonyesha ushirikiano na hii sio mara ya kwanza kufanya hivyo, tuna wajibu wa kuwapa furaha kabla ya mechi ya nyumbani,” alisema kocha huyo raia wa Brazili ambaye atamkosa winga Aubin Kramo ambaye aliyerejea kwenye majeruhi na kuwasha moto kwenye mechi tatu zilizopita za kirafiki. Mmoja wa watu wa benchi la ufundi, alilidokeza Mwanaspoti, Kramo ameumia goti na atakosa mchezo huo na hata ule wa marudiano kwa vile atakuwa nje kwa muda wa wiki mbili kabla ya kurudi uwanjani.
MASTAA WATAMBA
Mastaa wa timu hiyo walitamba wanaenda kuisaka heshima kwa klabu ugenini.
Beki Che Malone, alisema mchezo huo sio mwepesi na watacheza kwa bidii nakufuata maelekezo yote ya kocha.
“Sina cha kuahidi ila tunahitaji maombi zaidi twende na kurudi salama kwa vile matokeo ya soka hayatabiriki, ila tunataka kuipa timu heshima ugenini,” amesema Malone, huku Moses Phiri alisema wanakwenda kucheza mchezo mgumu ambao unahitaji matokeo mazuri kwa namna yoyote ile.
“Tunakwenda kucheza kwa heshima ili kupata matokeo mazuri ili tuweze kuingia hatua nyingine ya mashindano haya makubwa. Wachezaji na makocha tumejipanga kupata ushindi ili kuufanya mchezo wa marudiano uwe mwepesi kwetu,” amesema Phiri.