Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho aliwaweza Wydad, bado nafasi ipo

Simba Bomba Casablanca Robertinho aliwaweza Wydad, bado nafasi ipo

Tue, 25 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wasiwasi wa mashabiki wa Simba ni mechi ya marudiano dhidi ya bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad Casablanca huko Morocco wiki ijayo, ila mastaa wao wanaweza wakabadili upepo wakiamua iwe kufa na kupona ili kutinga hatua ya nusu fainali.

Mcheza kwao hutunzwa, ndivyo walivyoweza kuutumia vyema Uwanja wa Benjamin Mkapa mastaa wa Simba, wakiibuka kwa ushindi wa bao 1-0, lililofungwa dakika ya 30 Jean Baleke.

Bao hilo lilifungwa kwa utulivu mkubwa na Sadio Kanoute alipiga shuti kwa Kibu Denis ambaye aligeuka na kumpa pasi Baleke aliyetumbukiza mpira nyavuni na kuamsha furaha kwa Wanasimba, huku staa huyo akifikisha bao la nne CAF.

Haina ubishi Wydad ambayo imetwaa ligi ya mabingwa mara tatu, inatumia zaidi ufundi, mbinu, kuliko nguvu na mastaa wake ni wajanja wa kutengeneza faulo, wazuri wa mipira ya kutenga, hilo linapaswa kushughulikiwa na Kocha Roberto Oliveira kujua namna ya kuwakabili wapinzani wake kwenye robo fainali ya pili ugenini.

Roberto aliwahi kusema ataifikisha Simba nusu fainali kwenye michuano hiyo, ilikuwa kama kichekesho wakati huo, ila kwa sasa ni kama kauli yake inakwenda kutimia.

Pamoja na hilo, baadhi ya wataalamu wa soka wameona kitu kinachoweza kumbeba kocha huyo ugenini ni juu yake kukubaliana na ushauri wao ama anaweza akawa na jicho la kiufundi kujua nini kifanyike kushinda mchezo wa marudiano.

Pia Simba lazima ijue inakwenda kukutana na Wydad ambayo uwanja wao wa nyumbani kwenye mechi 10 za michuano hiyo imeshinda nane kutoka sare mbili.

Kati ya waliotoa ushauri huo ni kocha wa KVZ ya Zanzibar, Amri Said aliyesema ndani ya kikosi cha Simba kina mastaa wanaoweza kuamua mechi, kutokana na uzoefu wao wa kimataifa na wengi wao wanatumika timu zao za taifa, hivyo kocha analazimika kuwajengea kujiamini na kupandisha morali yao.

"Wengi wanaipima Simba na ligi ya ndani, ila wanasahau kimataifa ni bora zaidi, ina mastaa wengi wazuri ambao kocha anapaswa kuwajenga kiakili na kuwapa mbinu kulingana na nafasi zao, huku wakiangalia wapinzani wao ni wazuri eneo lipi.

"Roberto ana wachezaji wazuri sana baadhi ni kama Saidi Ntibazonkiza 'Saido', Ousmane Sakho, Baleke, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Kibu Denis, Henock Inonga, Joash Onyango, John Bocco bado anaimudu sana michuano, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shomari Kapombe hao ni baadhi."

Wakati huo huo, beki wa zamani wa timu hiyo Boniface Pawasa anaitazama nafasi ya Tshabalala na kumshauri wakati anapanda kushambulia anapaswa akumbuke jukumu lake la msingi la kukaba.

"Nawashauri wachezaji wa Simba, wasiende na matokeo ya kufungwa, waangalie marudio ya mchezo huo kwa manufaa ya kugundua makosa yao kisha wakafanye kwa ubora mchezo wa marudiano," anasema.

Ukiachana na hilo, Wydad ilionekana kuiheshimu Simba kwa kutokufunga sana kushambulia, ikitumia mfumo wa kujilinda zaidi wa 4-2-3-1 huku vijana wa Robertinho nao wakitumia mfumo huo huo huku wakionekana kushambulia zaidi.

Kwa mwaka huu Simba haina unyonge na mechi za ugenini kwani kwenye michezo mitano imeshinda mechi tatu na imefungwa miwili, jambo linaloweza likafanyika kwenye mchezo wao wa marudiano utakaopigwa Aprili 28.

Mabadiliko aliyoyafanya Roberto kumtoa Saido dakika ya 81 akimpa nafasi Sakho yalisaidia kuleta presha kwenye safu ya ulinzi ya Wydad kuna nafasi aliipata angeamua kupiga moja kwa moja huenda angepata bao lakini badala yake alianguka huku akionekana kuomba penalti.

Sakho ana kasi, lakini anapaswa kutumia akili zaidi kwenye maamuzi yake ya mwisho, ukimtofautisha na Saido ambaye alikuwa na jicho la kuona mbali mpenyo wa kufika golini lakini kasi yake na mikimiki haikuwa mikubwa.

Hata hivyo, kwenye mabadiliko ya kumtoa Beleke na kuingia nahodha John Bocco hayakuleta matokeo zaidi, inawezekana ilikuwa ni presha ya mchezo maana zilibaki dakika za mwisho na Wydad ilikuwa inafanya msako golini kwa Simba.

Kiufundi Wydad ilicheza kiufundi na kitimu, wakati Simba ilikuwa inaonekana kiwango cha mchezaji mmoja mmoja, mfano namna Chama alivyokuwa anaweza kufika ndani ya 18, Saido alivyokuwa anajaribu kupiga mashuti baada ya ukuta wa wapinzani wao kujenga ngome golini kwao.

WYDAD IKIWA KWAO

24/10/21 Wydad Casablanca 6 - 1 Hearts of Oak

11/02/22 Wydad Casablanca 3 - 0 Sagrada Esperança

26/02/22 Wydad Casablanca 3 - 1 Zamalek

03/04/22 Wydad Casablanca 5 - 1 Petro de Luanda

24/04/22 Wydad Casablanca 0 - 0 Belouizdad

13/05/22 Wydad Casablanca 1 - 1 Petro de Luanda

16/10/22 Wydad Casablanca 6 - 0 Rivers United

24/02/23 Wydad Casablanca 1 - 0 Petro de Luanda

03/03/23 Wydad Casablanca 1 - 0 Vita Club

02/04/23 Wydad Casablanca 3 - 0 Kabylie

28/04/23 Wydad Casablanca vs Simba mechi ijayo.

Chanzo: Mwanaspoti