Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema anataka kuona timu yake ikipata ushindi wa mabao mengi zaidi, huku akipanga kutengeneza muunganiko wa safu ya ushambuliaji na kiungo.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kumalizika kwa Simba kuwafunga Power Dynamos ya nchini Zambia mabao 2-0 yaliyofungwa na Willy Onana na Fabrice Ngoma.
Mchezo huo ulipigwa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika Tamasha la Simba Day. Onana anayecheza nafasi ya ushambuliaji na Ngoma kiungo, ni miongoni mwa nyota wapya kikosini hapo.
Akizungumza na Spoti Xtra, Robertinho alisema haikuwa rahisi kwa wachezaji wake kupata matokeo ya ushindi katika mchezo huo, hivyo anawapongeza kwa kushika maelekezo na mbinu zake mazoezini.
Robertinho alisema kilichobakia hivi sasa kwa wachezaji wake ni kuwatengenezea muunganiko mzuri kwa kuanzia safu ya kiungo kwenda kwa washambuliaji ili watengenezeane nafasi nyingi za kufunga mabao.