Zikiwa zimebaki siku nne kwa Simba kumaliza kambi maalumu nchini Uturuki, kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' ameshtukia kitu baada ya kiwango bora cha washambuliaji wake, akiwemo winga Kramo Aubin wa Ivory Coast.
Agosti Mosi, Simba inatarajia kufunga rasmi kambi hiyo iliyochukua wiki tatu nchini Uturuki na kurejea nchini tayari kwa mikiki ya 'Simba Day', Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na mashindano ya CAF, lakini hadi leo, Robertinho hajapata picha kamili atampanga nani katika eneo la usahambuliaji.
Kocha huyo raia wa Brazil alisema moja ya eneo ambalo hana shida nalo ni la mawinga na viungo washambuliaji, kwani ana zaidi ya wachezaji watano wanaweza kucheza maeneo hayo kwa ubora wa hali ya juu.
"Timu inaendelea vizuri, kila mchezaji ana morali ya juu na kila mtu anatimiza vyema majukumu yake kwenye eneo lake.
"Huenda msimu ujao tukawa na mabao mengi zaidi kutokana na safu ya ushambuliaji kuwa na watu wenye ubora mkubwa kuanzia akina Chama (Clatous) na Saido (Ntibanzokiza), waliokuwepo msimu uliopita, hadi hawa wapya, Kramo na Onana (Willy) kila mmoja ana kitu cha kipekee," alisema Robertinho.
Katika eneo la ushambuliaji, Simba ina jumla ya wachezaji 12, Kramo, Onana, Chama, Saido, Luis Miquissone, Moses Phiri, Kibu Denis, Jimmyson Mwanuke, Jean Baleke, John Bocco, Shaban Chilunda na Mohamed Mussa.
Wachezaji hao kwa ujumla msimu uliopita wamefunga mabao zaidi ya 80 kwenye mashindano yote, hivyo kwa mujibu wa Robertinho huenda safu yake ya ushambuliaji msimu ujao itazalisha mabao zaidi ya hayo.
Simba ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Turan FC, lakini kubwa zaidi imejiwekea mikakati ya kurudisha ufalme wake uliopotea kwa misimu miwili mbele ya Yanga, ambayo ilibeba kila kitu, Ligi Kuu, Kombe la FA (ASFC) na Ngao ya Jamii, hadi kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kutoka kapa katika misimu hiyo miwili kumeipa Simba hasira na kuamua kufanya usajili wa nguvu ikishusha wachezaji wapya 10, wakiwemo wazawa wanne, David Kameta 'Duchu', Husein Bakari 'Kazi', Abdallah Hamis, Shaban Chilunda na wageni sita, Che Malone Fondoh, Fabrice Ngoma, Miquissone, Kramo, Onana na kipa Jefferson Luis kutoka Brazil.
Wakati ikisajili wachezaji hao, Simba iliachana na Ismael Sawadogo, Jonas Mkude, Beno Kakolanya, Joash Onyango, Nelson Okwa, Erasto Nyoni, Victor Akpan, Habib Kyombo, Gadiel Michael, Agustine Okrah na Mohamed Ouattara.