Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho‘ ameweka wazi kwamba, tayari ana kikosi cha kwanza kilichokuwa tayari kwa mapambano ya mashindano yaliyo mbele yao, huku akihitaji muda zaidi kuupata muunganiko wa timu nzima ili kupata kikosi cha pili katika kuendeleza rekodi ya matokeo mazuri.
Robertinho ametoa kauli hiyo baada ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos uliochezwa juzi Jumapili kwenye Tamasha la Simba Day, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, huku Simba ikifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Willy Essomba Onana na Frabrice Ngoma.
Akizungumza nasi, Robertinho alisema licha ya kupata matokeo ya ushindi katika mchezo huo, lakini bado anahitaji muda wa kutosha ili kupata muunganiko wa timu yote kutokana na mashindano makubwa yaliopo mbele yao, huku akisisitiza kwa sasa anaweza kupata matokeo mazuri dhidi ya timu yoyote.
“Kambi yetu imetusaidia kwa sababu tumeweza kuimarisha eneo la kiungo, nilikuwa nina makundi mawili ya kuwasoma wachezaji, ukiangalia kama Ngoma amecheza vizuri japo haikuwa rahisi kutengeneza uelewano kwa timu mpya.
“Baada ya mchezo, nimeongea na Kibu (Denis), Saido (Ntibazonkiza) na Chama (Clatous) kuwa wamefanya ushirikiano bora na kupelekea kupata matokeo matuzuri.
“Sasa tunajiandaa na Supa Ligi, ukiangalia timu ya kwanza ipo tayari ingawa haiwezi kunifanya nibadili timu ya kwanza haraka japokuwa bado nahitaji muda zaidi wa kuijenga timu ya pili na kupata muunganiko wa timu nzima ambao utasaidia kuonesha soka ambalo ninalitaka lichezwe hapa kwa lengo la kupata matokeo mazuri katika michezo yetu,” alisema Robertinho.
Katika mchezo huo, kikosi kilichoanza kilikuwa hivi; Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Che Malone Fondoh, Henock Inonga, Sadio Kanoute, Willy Onana, Mzamiru Yassin, Kibu Denis, Saidi Ntibazonkiza na Clatous Chama.
Kikosi hicho kinaonekana ndicho kitakuwa chaguoa la kwanza kwa Robertinho wakati msimu wa 2023/24 ukianza, kabla ya hapo baadaye kubadilika kulingana na muunganiko wa timu utakapokuwa.