Kocha Mkuu wa Simba Roberto Oliveira 'Robertinho' ameipongeza timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kwa kufuzu Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) huku akimpa tano kiungo mshambuliaji wake Kibu Denis.
Robertinho amesema kwenye mchezo wa timu hiyo dhidi ya Algeria kikosi hicho kilicheza kwa nidhamu kubwa akimpongeza kocha wa timu hiyo Adel Amrouche na benchi lake.
"Nafikiri Tanzania ilicheza vizuri sana, walicheza kwa nidhamu ndani ya mchezo sio rahisi kufunga njia za timu bora kama Algeria," amesema Robertinho.
"Kufuzu kwa Tanzania kutaifanya Tanzania kuendelea kutambulika zaidi Afrika na Duniani, wachezaji walijituma sana nawapongeza pamoja na benchi nzima la ufundi,"
Aidha Robertinho amewakumbusha mashabiki wa soka kukumbuka kumpongeza kiungo wake mshambuliaji Kibu Denis akisema anaendelea kuwa na mchango mkubwa kiwanjani.
"Wakati nafika hapa kila shabiki alikuwa hafurahii wakiona Kibu anapewa nafasi ya kucheza, hawataki kuangalia mchango wake mkubwa ndani ya timu anayocheza.
"Sawa na Mzamiru anafanya kazi kubwa sana, Kibu alifanya kazi kubwa sana kwenye Ile mechi kuna wakati niliona amefunga bao zuri lakini sikujua kwanini limekataliwa.
"Watu wanatakiwa kukumbuka kumpongeza kuliko kusubiri kumlaumu pale anapokosea, ni mchezaji bora wa timu anayoitumikia uwanjani."