Droo ya michuano mipya ya African Football League (CAF Super League) ilifanyika juzi Jumamosi (Septemba 02) majira ya usiku, Simba SC ikipangwa kucheza na Al Ahly ya Misri na iwapo itavuka itakutana na mshindi kati ya Petro Luanda ya Angola au Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku Kocha Roberto Oliveira Robertinho akikiri ni mechi ngumu, lakini akisema ‘waache waje, tuone’.
Michuano hiyo inashirikisha timu nane na itazinduliwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 20 na kuifanya Simba SC iwe na siku 96 ngumu na za mtego.
Ila kama itafanikiwa kuchanga vyema karata itapata mzigo mkubwa wa fedha zitakazoipa jeuri hata ya kujenga na kumiliki Uwanja wa kisasa wenye hadhi ya kimataifa wa kuingiza mashabiki wasiopungua 25,000.
Mara baada ya Droo hiyo iliyofanyika Cairo, Msri, Robertinho amesema anajua Al Ahly ni timu kubwa na ngumu, lakini inafungika kwani Simba SC imeshaifunga mara kadhaa nyumbani, hivyo analipanga jeshi lake vyema kwa vita.
“Ni mechi ngumu, lakini mradi tupo kwenye michuano tunajipanga kupambana. Al Ahly inafungika, waache waje,” amesema Robertinho
Hii itakuwa ni mara ya saba kwa timu hizo kukutana kwenye michuano ya CAF tangu 1985, huku kila moja ikiwa na rekodi ya kushinda nyumbani.
Katika Droo hiyo ya Juzi Jumaosi (Septemba 02), TP Mazembe ya DR Congo imepangwa kucheza na Esperance ya Tunisia na mshindi atavaana na kati ya Enyimba ya Nigeria au Wydad Casablanca ya Morocco.
Mshindi wa Simba SC na Al Ahly atacheza na Mamelodi au Petro Luanda mechi za Nusu Fainali zitakazopigwa kati ya Oktoba 29 na Novemba Mosi.
Kama Simba SC ikifanikiwa kupambana vyema na ratiba ya kucheza mechi zisizopungua 15 za kimataifa na zile za Ligi Kuu kisha ikapata matokeo mazuri, klabu hiyo itajihakikishia kiasi cha takribani Sh31 bilioni kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mzigo ambao utaifanya iweke rekodi ya kuwa timu ya Tanzania iliyowahi kuingiza kiasi kikubwa zaidi cha fedha ndani ya muda mfupi.
Bingwa wa African Football League ataondoka na kitita cha Dola ll.5 milioni wakati ile inayotinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itapata kiasi cha Dola 900,000 (Sh2.3 bilioni).
Ratiba hiyo ngumu ambayo Simba SC iko mbele yake, inaanzia Oktoba l6 hadi Desemba 19 ambapo itakuwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na zile za African Football League.
Shughuli itaanzia Oktoba l6 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia ugenini katika mechi ya Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa na kurudiana nao jijini Dar es salaam, Oktoba Mosi ikivuka itaingia makundi.
Mechi za makundi zitachezwa nne kati ya Novemba 24 hadi Desemba 19 ambazo Simba SC akipata ushindi, itaingia Robo Fainali pasipo kutegemea mechi mbili za mwisho zitakazochezwa kati ya Februari na Machi mwakani.
Pia itakuwa na kibarua cha kuzisaka noti za Super League ambayo Fainali yake itapigwa Novemba Mosi.
Katika kipindi hicho cha siku 96 Simba SC itakabiliwa pia na kibarua kigumu cha michezo mitatu ya Ligi Kuu dhidi ya Young Africans, Prisons na Azam FC zinazoweka kuongezeka ikiwa Bodi ya Ligi (TPLB) itaamua pia kuipanga icheze viporo vya Coastal Union, Singida Big Stars, Mashujaa, Ihefu, Namungo, Tabora United, Kagera Sugar na Geita Gold.
Kocha ‘Robertinho’ amesema, wapo tayari kukabiliana na ratiba ngumu iliyo mbele.