Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliviera ‘Robertinho’ amesema atapangua kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca kwa kuwa anafahamu hata wapinzani wake watakuja tofauti.
Simba iliondoka juzi Jumatatu (April 24) majira ya jioni kwenda Morocco ikipitia Dubai kwa ajili ya mchezo wa pili wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kupigwa keshokutwa Ijumaa (April 28) baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es salaam.
Robertinho ambaye ameonekana kuwa na mbinu kali kwenye michezo ya hivi karibuni, amesema atafanya mabadiliko kwenye kikosi chake ili kuhakikisha anapata ushindi kwenye mchezo huo mgumu.
“Kutakuwa na mabadiliko ya kawaida ya kikosi, hili ni jambo la kawaida na wakati mwingine watu wanatakiwa kuzoea, tunakwenda na tahadhari kubwa kwa kuwa wapinzani wetu ni bora na watakuja tofauti na walivyocheza hapa nchini, lazima tukubali tunatakiwa kwenda kwa umakini mkubwa na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji.”
“Nafikiri maandalizi yetu, yanaonyesha tunaweza kufanya mambo makubwa ugenini, hakuna shaka kuhusu hilo, wachezaji tulionao ni bora na kila mmoja anafahamu umuhimu wa mchezo huo, jambo pekee ambalo tunatakiwa kufanya ni kuwa na tahadhari na kugundua tunakwenda kucheza ugenini siyo nyumbani,” amesema kocha huyo wa zamani wa Vipers ya Uganda.
Mbrazil huyo ameonekana kuwa na mbinu safi za ulinzi kwenye michezo miwili iliyopita na walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Young Africans kwenye Ligi Kuu Bara na kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Wydad AC, hivyo bado mashabiki wanaamini timu yao inaweza kuvuka kwenye hatua hii na kwenda Nusu Fainali.
Endapo Simba SC watafanikiwa kufuzu kwa Nusu Fainali itakuwa ni mara ya pili timu hiyo inafika hatua hiyo, lakini ikiwa imeshafika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho Barani humo.