Ni kama ameanza tambo Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, baada ya kusema kwa sasa anataka kuona wachezaji wake wakicheza soka zuri, huku akibainisha kwamba tayari ameanza kuona muelekeo wa kikosi chake kufanya kile anachokihitaji.
Robertinho ametoa kauli hiyo kufuatia Simba kufanikiwa kushinda mchezo wake wa pili wa Ligi Kuu Bara 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji na kufikisha pointi sita.
Akizungumza nasi, Robertinho alisema kwa sasa ameanza kupata muelekeo wa kikosi chake kwa kucheza soka ambalo amekuwa akitaka kuona linachezeka akiamini litakuwa ni sehemu yake kubwa ya kufikia mafanikio msimu huu.
Kocha huyo alisema nyota wapya na wale waliokuwepo awali wametengeneza muunganiko mzuri na kupata muelekeo wa timu yake kucheza soka la kushambulia mbele ya eneo la mpinzani kitu ambacho amekuwa akivutiwa nacho.
“Nahitaji kuona mpira mzuri, mpira sio ugomvi, ni kipaji na sanaa, napenda zaidi kushambulia zaidi na kucheza mpira mzuri, matarajio yangu muda mfupi naweza kupata muelekeo wa kile ninachokitaka katika kikosi changu, nimefurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wangu hasa wale tuliowasajili msimu huu wanaonesha kiwango bora na kadiri wanavyopata muda wa kucheza wanazidi kuimarika.
“Kadiri siku zinavyozidi kwenda wachezaji wanazidi kuzoeana, mimi nimetoka Brazil, nimecheza soka na sasa ni mwalimu, mara zote naamini kwenye soka la kushambulia pamoja na kumiliki mchezo na hicho ndicho ninataka wachezaji wangu wakifanye,” alisema Robertinho.