Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameweka wazi kuwa, anajivunia viwango bora ambavyo vinaendelea kuoneshwa na mastaa wapya wa timu hiyo akiwemo, Willy Esomba Onana na kuchimba mkwara mzito kuwa mastaa hao watafanya makubwa zaidi wakizidi kuzoeana.
Onana ambaye msimu uliopita aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda, ni miongoni mwa mastaa wapya wa Simba ambao wameanza na moto ndani ya kikosi hicho ambapo amefanikiwa kufunga bao moja katika mechi mbili.
Akizungumzia kasi ya nyota wao wapya waliosajiliwa msimu huu, Robertinko alisema: “Kwanza nawapongeza wachezaji wangu kwa kuendelea kujituma na kuipambania timu ili ipate mafanikio.
“Tuna kundi kubwa la wachezaji wageni ambao pia wameendelea kuonesha uwezo bora licha ya kwamba wengi bado hawajapata muda wa kutosha kucheza lakini kadiri siku zinavyoenda nafurahi kuona wanazidi kuimarika.
“Naamini baada ya kupata muda wa kuzoeana na wenzao watafanya makubwa zaidi ya haya wanayoyafanya sasa, wale ambao wameanza kufunga akiwemo Onana basi watafunga sana kwa kuwa tunaamini katika soka la kushambulia.”