Mashabiki wa Simba wanaendelea kufurahia burudani waliyoipata kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati timu hiyo ikiinyoosha Horoya AC ya Guinea kwa mabao 7-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' akitamka kauli ya kibabe mapemaa.
Kocha huyo alisema kutinga kwa Simba hatua ya robo fainali, hahofii kukutana na timu yoyote atakayopangwa nayo kwenye hatua hiyo, kwani atajipanga vyema kukabiliana na mpinzani yoyote.
Ushindi wa juzi usiku uliifanya Simba kutinga robo fainali ya michuano hiyo kutoka Kundi C na sasa inajiandaa kujua itakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini au Al Hilal ya Sudan za Kundi B, Wydad Casablanca ya Morocco au JS Kabylie ya Algeria zilizopo Kundi A ama Esperance au CR Belouizdad ya Algeria iwapo zitamaliza kama vinara wa makundi hayo baada ya ratiba kukamilishwa.
Hadi sasa Raja Casablanca ya Morocco ndiyo iliyojihakikishia kumaliza kama kinara wa kundi C na haiwezi kukutana na Simba iliyokuwa kundi moja kama ilivyo kwa timu zitakazomaliza nafasi ya pili kama wekundu hao na makundi yaliyosalia zinasubiriwa mechi za mwisho kujua msimamo ulivyo.
Hata hivyo, Kocha Robertinho aliliambia Mwanaspoti, ushindi huo haukuja kirahisi kwa vile waliwasoma vizuri Horoya na mapungufu yao kisha akawabadilishia mbinu kisha akawamaliza kwa kufumua safu ya ushambuliaji kwa kuwaanzisha wenye kasi huku akiwataka kupiga mashuti huku akiwataka kuanza kukabia juu.
"Tuliwasoma Horoya, niliumia walivyotufunga kule kwao, niliwaambia wachezaji wangu kwamba timu kubwa kama Simba haitakiwi kufanya makosa masra mbili tukawabadilishia mbinu zetu na wao wakaja kama walivyocheza kule," alisema Robertinho na kuongeza;
"Nilifurahia jinsi wachezaji wangu walivyopcheza kwa nidhamu kuanzia nyuma lakini kule mbele nadhani mliona tuliwapa nafasi watu ambao wana kasi na wanakimbia kutafuta mipira, niliwamabia mkifika lango la wapinzani pigeni mashuti wakitema malizieni."
Kuhusu droo ya robo fainali, kocha Robertinho aliyecheza na staa wa Brazili Romario alisema Simba haina wasiwasi na droo na kwamba watajipanga kumng'oa kigogo yoyote watakayekutana naye.
"Kitu bora kwasasa timu imeanza kuelewa mbinu zangu lakini pia hata mashabiki wanaanza kujua Robertinho ni nani, tunahitaji muda tu kutengeneza timu, Simba haiwezi kuhofia timu yoyote tunachoweza kufanya ni kuwaheshimu wapinzani wetu," alisema kocha huyo na kuongeza;
"Tuna muda wa kutulia na kujipanga vuzuri zaidi, kitu bora sasa kwetu ni kuwa na muendelezo wa kufanya vizuri, nafikiri droo ikifanyika tukijua tutakutana na yupi tutarudi kujipanga na kujua ni mbinu gani tuzitumie kushinda, hii ni timu kubwa hapa Afrika ndio maana tupo hapa."