Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho: Nimeshapata dawa ya Wazambia

Roberto Robertinho.jpeg Robertinho: Nimeshapata dawa ya Wazambia

Wed, 13 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku tatu zikisalia kabla ya mchezo wao wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Raundi ya Kwanza, Kocha Mkuu wa Simba SC, Robertinho Oliveira, amesema tayari ameandaa dawa kwa ajili ya wapinzani wao, Power Dynamos na watawashangaza wakiwa nyumbani kwao Ndola, Zambia.

Simba SC itakuwa mgeni wa Power Dynamos Jumamosi (Septemba 16) kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Robertinho amesema wapinzani wao hao wasitegemee kuiona Simba SC waliyocheza nayo kwenye tamasha la Simba Day Agosti 6, mwaka huu, kwani katika mchezo huo utakaochezwa Jumamosi (Septemba 16), wataingia Uwanjani tofauti.

“Mchezo tuliokutana nao siku ya Simba Day likuwa na makusudio tofauti, huu wa Septemba 16, mwaka huu nao ni tofauti, huu ni mchezo wa maamuzi, nimetumia muda kuwasoma wapinzani wetu na tayari mikakati yangu imekaa sawa tunasubiri siku ya mchezo,” amesema Robertinho.

Katika mchezo huo wa kirafiki ambao Power Dynamos walialikwa, Simba SC ilibuka na ushindi wa mabao 2-0, mabao ya Willy Onana na Fabrice Ngoma.

Amesema utofauti kwenye mchezo wa Jumamosi (Septemba 16) utaanzia kwenye aina ya wachezaji atakaochagua kuanza katika mchezo huo na aina ya mfumo atakaoutumia.

“Hautakuwa mchezo mwepesi kwa sababu wapinzani wetu nao wamejiandaa, lakini Simba SC ni timu kubwa yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa na lazima tulionyeshe hili, tutatumia siku hizi chache zilizobaki kumalizia maandalizi yetu ambayo kwa kiasi kikubwa tumefika mbali, tunaomba tu sapoti ya mashabiki wetu,” amesema Robertinho

Amesema kwa ratiba ilivyo wanatarajia kuondoka nchini kesho Alhamis (Septemba 14) kuelekea Zambia tayari kwa mchezo huo na watarejea haraka kujipanga kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utathibitishwa timu itakayofuzu hatua hiyo ya makundi.

Kama Simba SC itafanikiwa kutinga hatua ya Makundi itakuwa mara ya tano kwenye michuano hiyo tangu msimu wa 2019-2020.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live