Kocha Mkuu Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ ametoa ufafanuzi baada ya kuutaka Uongozi kuhakikisha unasajili Mshambuliaji mpya, agizo lililoleta mkanganyiko miongoni mwa Mashabiki na Wanachama, ambapo baadhi yao walidai huenda hapendezwi na uwezo wa Mshambuliaji John Raphael Bocco.
Robertinho aliyeanza kazi rasmi mwishoni mwa juma lililopita baada ya kikosi chake kuweka Kambi Dubai-Falme za Kiarabu, alitoa agizo hilo siku moja baada ya kujiridhisha ubora na udhaifu wa kikosi chake.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema hakumaanisha kuwa Bocco hana uwezo wa kuipambania Simba SC, na huenda watu wengi walimuelewa tofauti hasa kwa maagizo aliyoyatoa kwa viongozi.
Amesema Mshambuliaji huyo mzawa ana uwezo mkubwa na amebaini anaweza kuipambani timu kwa kutumia uzoefu wake, lakini ameagiza asajiliwe Mchezaji mwingine anayecheza nafasi yake, ili kuleta ushindani wa nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Nimemuangalia Bocco kwa siku hizi chache na kujiridhisha kuwa ni miongoni mwa wachezaji bora na mwenye uzoefu mkubwa kutokana na kucheza kwa muda mrefu,”
“Lakini siku zote ili kuwa bora zaidi unapaswa kuwa na mshindani atakayekupa changamoto ya kupambana zaidi, hivyo nimewaomba viongozi tufanye maboresho katika eneo hilo kwa kusajili mchezaji mwingine ambaye watapeana changamoto.” amesema Kocha Robertinho
Simba SC imeweka kambi Dubai-Falme za Kiarabu ikijiandaa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Ikiwa huko Simba SC itacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Dhafra FC ya UAE na CSKA Moscow ya Urusi.
Simba SC itaanza kucheza mchezo wake wa kwanza wa Kirafiki kesho Ijumaa (Januari 13) dhidi ya Dhafra FC majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa za Tanzania, na Jumapili (Januari 15) itacheza dhidi ya CSKA Moscow iliyoweka kambi ya maandalizi Dubai.