Kocha Mkuu wa Klabu ya Soka ya Simba, Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo, maarufu kama Robertinho amesema kuwa kikosi chake kwa sasa kinacheza vizuri sana tofauti na mashabiki wanavyolalamika.
Robertinho amesema hayo jana Alhamisi, Septemba 21, 2023 mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Coastal Union huku Simba wakiibuka na ushindi mnono wa bao 3-0 katika Dimba la Uhuru.
Robertinho amesema kuwa kiungo wake mshambuliaji, Luis Jose Miquissone ameanza kuiva na kurejea kwenye ubora wake alioondoka nao Simba mwaka 2021, hivyo ana uhakika timu yake itakuwa imara muda si mrefu.
"Miquissone sasa ameiva, amecheza dakika 90 na ameonyesha kiwango bora sana leo, hii ndio msingi wa timu yangu ninaoutaka kwa ajili ya Simba tishio siku zijazo.
"Sote tunakumbuka alivyokuwa wakati anakuja, umbo lake lilikuwa kubwa kwa hiyo ni kazi imefanyika kuhakikisha anarejea kwenye hali yake na ubora wake wa zamani. Ninawapongeza wachezaji wangu wote wamecheza vizuri sana.
Kwenye soka unaweza kuingia na mbinu ya kutumia pasi, kumiliki mpira, kutumia nguvu ama kutumia vijana wenye vipaji, kikubwa upate matokeo. Nilichopwatuma wachezaji wangu ndicho walichokitekeleza, Simba ijayo itakuwa balaa," amesema Robertinho.