Ushindi mtamu nyie! Unaambiwa kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' ametoa tambo saa chache baada ya ushindi wa mabao 3-1 iliyopata ugenini mbele ya Tanzania Prisons akisema kwamba kazi ndio imeanza na kwamba kila watakayekutana lazima wajipange vinginevyo watazichezea nyingi.
Simba ilipata ushindi huo kwenye pambano kali lililopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya ambapo wenyeji Prisons ndio iliyotangulia kupata bao dakika ya 12 tu kupitia Edwin Balua kabla ya Simba kuzinduka na kusawazisha kwa bao la Clatous Chama kisha John Bocco akaongeza la pili kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili Simba iliwakimbiza maafande hao na kupata bao la tatu kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Saido Ntibazonkiza na kuifanya timu hiyo kuvuna pointi tatu na kupaa hadi kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 12, ikiing'oa Azam iliyo na pointi 10 na usiku wa leo Ijumaa inashuka uwanjani kuvaana na Coastal Union, jijini Tanga.
Ushindi huo wa Simba umekuja huku kukiwa na kelele nyingi kwa Robertinho anayelalamikiwa kwa kushindwa kuifanya timu ipige Pira Biriani kama zamani licha ya kupata matokeo mazuri, lakini kocha huyo raia wa Brazili amesema kazi ndio imeanza na timu yoyote itakayozubaa itapigwa nyingi ili kutimiza malengo.
Kocha Robertinho amesema licha ya ugumu wa Prisons timu yake imeonyesha ukomavu mkubwa ikitoka nyuma kwa kufungwa bao moja kisha kurudisha na kushinda mchezo huo.
Robertinho amesema, tayari kikosi chake kimeendelea kuonyesha utulivu na muunganiko wakicheza bila presha na kutengeneza ushindi hatua ambayo wanataka kuiendeleza zaidi.
"Sio kila timu itaweza kucheza kama hivi ilikuwa mechi ngumu dhidi ya Tanzania' Prisons, kitu bora zaidi ni jinsi tulivyotoka nyuma na kutengeneza ushindi huwezi kufanya hivyo kama huna wachezaji bora na mbinu sahihi," amesema Robertinho na kuongeza;
"Simba tunacheza soka bila presha hivi ndivyo ninavyotaka tucheze msimu huu, nawapongeza sana wachezaji wangu wamewapa mashabiki wao kile walichotarajia Sasa tunatakiwa kuiendeleza hii kwa kushinda zaidi kwenye michezo iliyopo mbele yetu kutimiza lengo la kurejesha mataji."
Pia Robertinho amefunguka kwamba ana wasiwasi na uchovu wa wachezaji wake kuweza kuwaathiri kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Singida Big Stars watakaokutana nao keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Simba imesharejea jijini Dar es Salaam na kesho mchana itasafiri kwenda Singida ikipitia Dodoma tayari kwa mchezo huo wa Jumapili, ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 kwenye mchezo wa msimu uliopita.
"Tuna ratiba ngumu kweli, unaona tumelazimika kurudi usiku huu, wachezaji watapumzika masaa machache na baada ya hapo tutaanza safari ya kwenda Singida, kitu kibaya hapa tunakosa muda wa kufanya mazoezi ya kurudisha utulivu wa mwili na tutakuwa na siku moja pekee ya kujiandaa na mchezo ujao," alisema Robertinho aliyeweka rekodi ya kibabe tangu atue Simba akiiongoza mechi 15 za Ligi Kuu bila kupoteza, akishinda 13 na kutoka sare mbili, lakini akiwa tayari ameshatwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga katika fainali iliyopigwa Agosti 13 jijini Tanga.