Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Riwaya ya Zahera inavutia mwanzoni

49827 ZAHERA+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa pamoja tuliwahi kuungana kuwa hakukuwa na maajabu yoyote ambayo klabu ya Yanga ingeweza kufanya msimu huu, mpaka pale alipotua ndugu yetu Mwinyi Zahera. Kuanzia ‘mushkher’ za msaada wa Feisal Salum “Feitoto” kutoka kwa Mwigulu Nchemba, sakata la Mwenyekiti Manji mpaka bajeti nzima ya klabu hiyo.

Ulikuwa ukitazama kikosi pia, waliotegemewa walikuwa na umri wa majeruhi yasiyokwisha wa Amissi Tambwe huku hata Papy Tshishimbi aliyewahi kuweka nuru kwenye nyuso za wengi akianza kuwa giza totoro. Kulikuwa na sababu nyingi za ndani na nje ya uwanja ambazo zingeweza kukufanya uamini kuwa Yanga ilikuwa haiepuki windo la nyuki hasa ukikumbuka pia kuwa fedha haikuwa ndugu yao msimu huu. Fedha ilikuwa mpenzi wa muda mrefu wa Yanga aliyeamua kuwa msaliti.

Wimbo ulibadilika kiitikio baada ya Zahera kutuonyesha Ibrahim Ajibu tuliyekuwa tunatamani kumwona miaka mingi akicheza kwa mwendelezo, Feisal ambaye angeweza kuanza mbele ya wenye ndevu nyingi na Yanga ikawa kile wanachoita “Ngoma Inogile.” Hata walioamua kutaka kuchangisha au kupitisha bakuli haikuwa ngumu na ilipata muitikio kwa sababu ya mwanaume mmoja anaitwa Zahera.

Hizo zikiwa kurasa za mwanzo za riwaya ya Yanga bila Manji, inawezekana kabisa Zahera akawa chachu ya uandishi mzuri wa kitabu kizima na kila kurasa yake ikawa inavutia kusoma. Makocha kama Zahera wakiwa na misimamo na wakaepuka kuingia kwenye siasa za kimjini mjini hapa Tanzania wanaweza kuwa chachu ya mafanikio kwa klabu hizi. Tatizo pekee ni kuwa misimamo hii huwa haidumu na roho hizi hugeuka mara moja. Sina tatizo iwapo Yanga haitaweza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sina tatizo Yanga ikiondolewa kwenye kombe la TFF, nitakuwa na tatizo tu kama klabu hiyo ikishindwa kujijenga kutokea hapa ilipowekwa na Zahera. Ukiona jasiri mwenye njaa anapigana vita usiku, basi pakikucha atahitaji japo matunda ya porini kuendelea kupambana na kushinda vita yako.

Yanga wanahitaji kwa haraka kutambua hili, wanahitaji kufahamu ujasiri wa Zahera unaweza kuwa na kikomo, hivyo yawapasa kusimama na kufahamu wanaelekea wapi na wanatumia usafiri upi kufika wanakokwenda. Mbio za gizani haziwasaidii kwani kujikwaa na kuumia haliwezi kuwa jambo la ajabu, kuanguka kwao hakutamstua mtu na hata majeraha yao hayatamsikitisha binadamu yeyote mwenye akili timamu. Mfumo rasmi unahitajika Yanga, mfumo utakaotoa mwanga wa timu inachukua hatua zipi kujikimu na si kuzungusha bakuli. Kocha wa kusimamia maisha ya wachezaji na kupata kilicho bora kutoka kwao tayari wanaye lakini atahitaji kuungwa mkono. Viongozi na wanaotaka kuwa viongozi na wanaozuia uongozi wanatakiwa kufahamu kuwa kisigino hata ukipende vipi huwezi kukiweka mbele na tabia yao ya kupenda kutembea kwa kurudi nyuma, si maisha ya binadamu. Hatukuumbwa tukiwa na gia ya rivasi na ndio maana macho hayapo kisogoni.

Wenye hekima wasimame, waitetee Yanga wenye upendo watulie waisaidie Yanga na wezi waondoke wasiinyong’onyeze klabu ya wananchi. Yanga ina mtu sahihi ambaye bahati nzuri amekuwa kipenzi cha mashabiki, mtu ambaye amefahamu mazingira ya klabu kwa haraka na mtu ambaye anatangaza kujenga kila mara na kuweka msimamo chanya ndani ya mioyo ya mashabiki, wachezaji na hata vyombo vya habari. Muda bado upo na Yanga haijachelewa kuanza kujiuliza misimu miwili ijayo maisha yatakuwaje, msimu ujao Yanga itasimama vipi na tutawezaje kuwasimamia akina Feisal na Paul Godfrey wasitamani kwenda kwingineko. Ni raha kwelikweli kusoma riwaya hii mwanzo na inaleta matumaini, funzo na hamu ya kutaka kufahamu ni mazuri yapi yanayofuata, nini mikakati ya muda mrefu yenye kuendana na kocha huyu lakini kurasa za katikati na mwisho bado zipo tupu, hazijatendewa haki. Yanga ndani ya uwanja imeonyesha ukiwa na mipango na watu sahihi unaweza kuishi maisha ya soka na ukaeleweka, nje ya uwanja bado hakuna watu wanaoendana na jina la klabu yenyewe.

Umefika wakati wa kwenda na mabadiliko ya tabia soka ambayo yanatokana kwa kiasi kikubwa na sayansi ya soka na ugunduzi ambao unachochea kila kitu kusimamiwa kisasa zaidi. Binafsi Zahera amenishawishi ndani ya uwanja, nimependa Riwaya anayoandika, lakini bila klabu kusukwa na kusimama imara, hataweza kujaza kurasa nyingi zilizobaki.



Chanzo: mwananchi.co.tz