Kiungo wa zamani wa Real Madrid na nahodha wa timu ya taifa ya Colombia Freddy Rincon amefariki dunia leo kwenye hospital ya Imbanaco mjini Cali nchini Colombia alipokuwa anapatiwa matibabu baada ya kupata ajali mbaya ya kugongana na basi siku ya jumatatu.
Rincon mwenye umri wa miaka 55 aliichezea Colombia kwenye fainali 3 za kombe la dunia ( 1990, 1994 na 1998) na kuifungia magoli 17 huku akipita kwenye vilabu vya Real Madrid,Napoli, Palmeiras ,Santos sambamba na klabu ya Corinthians ya Brazil.
"kwa juhudi zote walizozifanya madaktari tunapenda kuwatarifu kwamba Freddy Eusebio Rincon Valencia amefariki dunia "amesema mkurugenzi wa hospitali ya Imbanaco ,Laureano Quintero kwenye taarifa kwa umma mapema leo asubuhi
Vilabu na masharikisho mbalimbali ya soka duniani yametoa salamu za pole kutokana na msiba huo huku chama cha soka cha Colombia (FCF) kimeomboleza kwa kuandika "tutamkumbuka na kumuenzi kwa uongozi ,mchango na heshima yake kubwa kwenye timu ya taifa na tunatoa salamu za pole kwa familia na tunaamini watapita katika kipindi hiki kigumu wanachokipitia kwa sasa".