Wakati mashabiki wa Arsenal wakiwa hawaelewi ikiwa wanaweza kuipata huduma ya kiungo wa West Ham Declan Rice baada ya ofa zao mbili kukataliwa wamepewa ujanja ambao utawawezesha kufanikisha usajili wa fundo huyo.
Mchezaji wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya England Danny Murphy amesisitiza kwamba Rice mwenyewe anatakiwa aanzishe mtiti wa kutaka kuondoka lasivyo ataendelea kusalia kwenye kikosi hcho.
Arsenal hadi sasa imewasilisha ofa mbili kwa ajili ya staa huyu na yamwisho ilikuwa inafikiia Pauni 90 milioni lakini West Ham imeendelea kusisitiza kwamba inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 100 milioni.
Kabla ya msimu uliopita kumalizika, Mwenyekiti wa West Ham David Sullivan alimwambia Rice kwamba katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Hata hivyo inaonekana bei ambayo ilipangwa kumuuzia kwa mara kwanza imepanda zaidi hasa baada ya thamani ya staa huyu kuongezeka baada ya kuiongoza West Ham kushinda taji la Europa Conference League yeye akiwa ndio kapteni.
Hadi sasa timu inayoonekana kuwa tayari kutoa pesa na kumsajili ni Arsenal peke yake lakini kitendo cha West Ham kuendelea kushikilia msimamo wa kutaka kumuuza kwa bei kubwa zaidi fundi huyu huenda akaishia kubakia kwenye kikosi hicho.
Akizungumza na TalkSport Murphy alisema:"Hadi sasa Man City haionekani kuwa kwenye vita, hivyo hata Arsenal pia inaonekana kuwa inaenda taratibu kwani hakuna upinzani, hapo sasa ndio Declan anatakiwa atumie ushawishi kulazimisha kuondoka ikiwa anahitaji, unahitaji kuwa mtukutu kama Craig Bellamy ama Joey Barton(Utukutu), inabidi ujiangalie mwenyewe, nafasi kama hizi huwa zinakuja mara moja moja sana kwenye maisha ya wachezaji."
Mwaka 2010, Bellamy alilalizimisha kuondoka Man City na matokeo yake timu ilishindwa kuzuiwa na akaruhusiwa kuondoka kujiunga na Cardiff kwa mkopo kabla ya kutua Liverpool ambako ndio ilikuwa lengo lake haswa.
Wachezaji wanapokuwa wanalazimisha kuondoka mara nyingi timu zao zinazotaka kuwabakisha hushindwa na kujikuta zinawauza kwani hata zikiwabakisha huona huenda wasiwape kile ambacho wanachohitaji kwa sababu ya kushuka kwa hali ya kuipambania timu.
"Inatakiwa uiambie tu timu kwamba mkiendelea kushikilia hapa kwakeli sitocheza, licha ya kwamba moyo wako utakuwa unafikiria kucheza lakini itabidi uwaambie na kuwaamisha kwamba ni kweli unachosema.'' Rice ni miongoni mwa mastaa ambao huduma zao zinawindwa sana kutokana na kiwango alichoonyesha kwa msimu wa tatu sasa tangu aibuke akiwa na West Ham.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2024, lakini West Ham ina jeuri kwa sababu kuna kipengele cha kuurefusha kwa mwaka mmoja ikiwa watahitaji kufanya hivyo. Kwa msimu uliopita staa huyu alicheza mechi 50 za michuano yote na akafunga mabao matano na kutoa asisti nne.
Hata hivyo bado Arsenal inaonekana kuwa kwenye mpango wa kutaka kuwasilisha ofa nyingine kwa ajili ya fundi huyu ingawa haitazamiwi kuwa sawa na ile ya Pauni 100 milioni ambayo West Ham wanaihitaji. Mashabiki wengi wa West Ham wameonekana kumjia juu Murphy wakidai kwamba ana chuki nao kwa kuwa aliwahi kucheza Tottenham Hotspur ambayo ni timu hasimu ya West Ham.