Rekodi sifa yake ni kuvunjwa, lakini hizi 20 za Ligi Kuu England zitachukua muda mrefu sana kuvunjwa.
Mashabiki wa soka wamepata kushuhudia rekodi mbalimbali kwenye Ligi Kuu England. Ligi hiyo ya soka kubwa kabisa huko England ilianzishwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, ikishuhudiwa wachezaji na makocha mahiri kabisa wakipita na kuacha alama.
Manchester United iliweka utawala wake miaka ya mwanzoni, wakati Arsenal, Chelsea na Manchester City kila moja ina zama zake. Leicester City iliingia kwenye rekodi kwa kubeba ubingwa wa ligi kwa staili isiyotarajiwa kabisa.
Lakini, Ligi Kuu England sio ishu ya kubeba ubingwa tu. Historia inaweza kuwekwa kwenye nyanja nyingi, ambapo zinaweza kuwa nzuri au mbaya. Kuna hizi rekodi 20 kwenye Ligi Kuu England, ambazo huoni kama zitakuja kuvunjwa kwa miaka ya hivi karibuni.
1. Hat-trick tatu kwenye mechi chache
Rekodi hiyo ni ya mechi nane na inashikiliwa na straika Erling Haaland, aliyoweka msimu wa 2022/23. Haaland alitua England kwenye majira ya kiangazi 2022 na tangu wakati huo amekuwa akifunga tu, akiweka rekodi ya kufunga hat-trik tatu katika mechi nane, ikiwa ni mechi chache zaidi kuwahi kutokea.
Alifunga hat-trick ya kwanza dhidi ya Crystal Palace, kisha Nottingham Forest na kufuatia Manchester United. Kabla ya hapo, rekodi hiyo ilikuwa inashikwa na Michael Owen, hat-trick tatu kwenye mechi 48.
2. Kugongesha mwamba mara nyingi mechi moja
Rekodi hiyo ni ya kugonga mwamba mara nne, inashikiliwa na Darwin Nunez wa Liverpool, aliyofanya kwenye mechi dhidi ya Chelsea, Jumatano iliyopita. Katika mchezo huo, Darwin Nunez - ambaye amekuwa akishutumiwa kwamba hatumii vyema nafasi zake anazopata tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Anfield, alikuwa na bahati mbaya kwenye mechi ya Chelsea, baada ya kugongesha mwamba mara nne na kuweka rekodi hiyo tamu ambayo itachukua muda mrefu kuvunjwa. Chelsea ilichapwa 4-1.
3. Mechi mfululizo bila ya kupoteza
Rekodi ni ya mechi 49, inayoshikiliwa na Arsenal ambayo iliweka kati ya Mei 7, 2003 hadi Oktoba 24, 2004. Rekodi tamu zaidi ya Arsenal kwenye Ligi Kuu England ni ile ya kucheza msimu mzima bila ya kupoteza. Lakini, kama hiyo haitoshi, timu hiyo ya Emirates inashikilia rekodi pia ya kucheza mechi nyingi mfululizo bila ya kupoteza, ikicheza mechi 49 bila ya kupoteza. Rekodi hiyo ilikwenda kuvunjwa na Manchester United katika mchezo wao wa 50, ambapo Arsenal ya Arsene Wenger ilikubali kichapo.
4. Kucheza mechi nyingi mfululizo
Rekodi ni mechi 310, ambayo inashikiliwa na kipa wa zamani Brad Friedel, aliyecheza mfululizo kuanzia Agosti 14, 2004 hadi Septemba 29, 2012. Kutokana na upana wa vikosi na mtindo wa kubadilisha wachezaji kila mara jambo hilo linaonekana kuwa gumu kwa mchezaji mmoja kucheza mechi 310 mfululizo. Kufanya rekodi hiyo kuwa ya kipekee, Friedel si kwamba kwa misimu hiyo minane alikuwa kwenye timu moja, alipita Blackburn Rovers, Aston Villa na Tottenham Hotspur na kucheza mfululizo kufikisha mechi hizo.
5. Pointi chache zaidi kwenye msimu
Rekodi ni pointi 11, ambazo zilivunwa na Derby County katika msimu wa 2007/08. Bila shaka Derby itakuwa inapiga sala kila msimu wa Ligi Kuu England ili itokee timu itakayovuna pointi chache zaidi ya 11, ambao wao waliwahi kuzipata na kuweka rekodi hiyo ya hovyo. Kwa hali ilivyo, rekodi hiyo ya Derby huenda ikachukua muda mrefu sana kuvunjwa kwa maana ya timu kupata pointi chache kiasi kama hicho cha pointi 11 ili kuvunja rekodi hiyo ya kibabe kabisa.
6. Vipigo vingi mfululizo
Rekodi hiyo ni vipigo mfululizo kwenye mechi 20 na wanaoshikilia ni Sunderland, waliweka kuanzia 2003 hadi 2005. Derby ilipata sare chache sana katika msimu wao mbaya kwenye Ligi Kuu England, lakini Sunderland walikuwa kwenye majanga zaidi kwenye ligi hiyo. Miamba hiyo ilipoteza mechi 15 za mwisho kwenye msimu wa 2002-03, ikashuka daraja. Ilipanda na kurejea kwenye Ligi Kuu England mwaka 2005, ilipoteza mechi tano za kwanza na hivyo kuweka rekodi hiyo ya kupoteza mechi 20 mfululizo.
7. Mchezaji mwenye umri mkubwa
Rekodi ni umri wa miaka 43 na siku 162 na inashikiliwa na John Burridge wa Manchester City aliyoweka alipopangwa kwenye mechi dhidi ya QPR, Mei 14, 1995. Rekodi ya kipa huyo kwa soka la kisasa, haitakuwa rahisi kuvunjwa kwenye Ligi Kuu England. Burridge alidaka kwenye mechi akiwa na umri wa miaka 43. Sawa, wachezaji wana uwezo wa kucheza muda mrefu kuzidi wachezaji wa ndani, lakini kwa hali ilivyo kwenye Ligi Kuu England kwa kasi ya soka la kisasa, itakuwa ngumu kwa rekodi yake kuvunjwa kirahisi.
8.Ubingwa kwa tofauti ndogo ya pointi
Rekodi ni pointi 0 na kwamba bingwa alibeba kwa tofauti ya mabao manane, ambao ni Manchester City katika msimu wa 2011/12, ilipowazidi mahasimu wao Manchester United na kuwapiga kikumbo kwenye ubingwa wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya mabao manane tu. Kwa msimu huo, ubingwa uliamuliwa siku ya mwisho ya msimu, ambapo kumbukumbu nzuri ni lile bao la dakika za mwisho la Sergio Aguero kwenye mechi dhidi ya QPR baada ya pasi matata ya straika Mario Balotelli. Hapo Man City ikanasa ubingwa wake wa kwanza.
9.Bao la haraka zaidi
Rekodi ni sekunde 7.69. Anayeshikilia ni Shane Long wa Southampton, aliyefunga katika mchezo dhidi ya Watford, Aprili 23, 2019. Unaweza usiamini kwamba bao linaweza kufungwa kwa haraka hivyo, lakini kwenye Ligi Kuu England, Shane Long anashikilia rekodi ya kufunga bao baada ya sekunde ya saba tu mechi kuanza. Hakuna bao jingine lililofungwa mapema kuzidi hilo hadi sasa kwenye Ligi Kuu England na kufanya jambo hilo liendelee kuwa rekodi inayoonekana itachukua muda mrefu kuvunjwa.
10. Pointi chache za ubingwa kwa msimu
Rekodi ni pointi 75, ambazo ilivuna Manchester United katika msimu wa 1996/97 na kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England. Wakati Manchester City na Liverpool kwa miaka ya hivi karibuni zikipambana na kufikisha au kukaribia pointi 100 ndipo ziwe na uhakika wa kunyakua ubingwa wa ligi, huko nyuma Ligi Kuu England iliwahi kutoa bingwa kwa mwenye pointi 75 tu, ambapo Man United ilizivuna na kubeba taji. Msimu wa 2017-18, Man City ilipobeba na pointi 100, timu yenye pointi 75 ilishika nafasi ya nne.
11.Mechi nyingi nyumbani bila ya kupoteza
Rekodi ni mechi 86 na inashikiliwa na Chelsea, waliocheza bila ya kupoteza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Stamford Bridge kuanzia Machi 20, 2004 hadi Oktoba 5, 2008. Rekodi hiyo ya Chelsea ilivunjwa na Liverpool kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, shukrani kwa shuti la Xabi Alonso. Miaka ya hivi karibuni, Liverpool na yenyewe ilikuwa ikifukuzia rekodi hiyo ya kucheza mechi nyingi nyumbani bila ya kupoteza, lakini ilikomea mechi 69, mechi 17 pungufu ya kufikia rekodi ya The Blues.
12.Mashabiki wachache zaidi uwanjani
Rekodi ni mashabiki 3,039 - waliohudhuria mechi ya Wimbledon na Everton, Januari 26, 1993. Katika kipindi kichohususisha zuio la mashabiki kuingia uwanjani kwa wingi katika kipindi cha janga la uviko-19, mechi ya Wimbledon na Everton ndiyo inayoshikilia rekodi ya kuhudhuriwa na mashabiki wachache zaidi uwanjani kwenye historia ya Ligi Kuu England, ambao hawakufika hata mashabiki 3,100. Hakuna mechi katika msimu wa kawaida itakuwa na mashabiki chini ya 3000 ili kuvunja rekodi hiyo.
13.Hat-trick ya haraka zaidi
Rekodi ni dakika 2 na sekunde 56. Na anayeshikilia rekodi hiyo ni Sadio Mane, aliyefunga hat-trick wakati yupo Southampton katika mechi dhidi ya Aston Villa, iliyopigwa Mei 16, 2015. Wakati Haaland akionekana kama mkali wa hat-trick, lakini uhodari wake wote bado hajavunja rekodi ya Mane ya kufunga mabao matatu ndani ya mechi moja na kutumia muda mchache zaidi, dakika 2 na sekunde 56. Robbie Fowler aliwahi kufunga hat-trick kwa dakika 4 na sekunde 32 mwaka 1994, Liverpool dhidi ya Arsenal.
14. Kucheza muda mrefu bila ya kuruhusu bao
Rekodi ni dakika 1,113 na anayeshikilia ni kipa Edwin van der Sar wakati alipokuwa akikipiga kwenye kikosi cha Manchester United, ambapo alidaka kuanzia Novemba 15, 2008 hadi Februari 18, 2009 bila ya kuruhusu bao. Rekodi hiyo bado haijavunjwa na huenda ikachukua muda mrefu. Kipa huyo wa Kidachi, katika msimu wa 2008-09, alidaka mechi 14 mfululizo bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa. Mtu aliyekuja kutibua rekodi yake ni staa wa Blackburn, Roque Santa Cruz. Petr Cech akiwa Chelsea alikomea dakika 1,025.
15. Kufunga bao kwa misimu mfululizo
Rekodi ni misimu 21 na anayeshikilia ni Ryan Giggs, ambapo kuanzia msimu wa 1992/93 hadi 2012/13, alifanikiwa kufunga bao katika kila msimu. Suala la kucheza misimu 21 mfululizo kwenye Ligi Kuu England yenyewe tu ni rekodi tamu bila ya kujumuisha kufunga bao katika kila msimu. Kwa kifupi tu, Giggs alifunga bao kwa misimu 23 mfululizo, lakini misimu miwili ya kwanza ilikuwa kabla ya Ligi Kuu England haijaanza. Winga huyo aliendelea kuzitesa nyavu za Ligi Kuu England hadi msimu wa 2012/13.
16.Mchezaji kufunga mabao mengi kipindi kimoja
Rekodi ni mabao matano na anayeshikilia ni mshambuliaji Jermain Defoe, aliyefanya hivyo alipokuwa kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur katika mchezo dhidi ya Wigan Athletic, Novemba 22, 2009. Hiyo ni rekodi nyingine ambayo Haaland atapambana kuivunja, ambapo Defoe alifunga mabao matano ndani ya dakika 45 tu za kipindi kimoja, wakati Spurs iliposhinda mabao 9-1. Mwingereza huyo alikuwa hashikiki kwenye mchezo huo na hakika Wigan watakuwa wamemweka kwenye kumbukumbu zao za kudumu.
17.Kocha kufundisha timu moja kwa muda mrefu
Rekodi ni miaka 21 na siku 224, inayoshikiliwa na Arsene Wenger, ambapo alianza kuinoa Arsenal kuanzia Oktoba 1, 1996 hadi Mei 13, 2018. Kwenye Ligi Kuu England kwa sasa, Jurgen Klopp wa Liverpool ndiye kocha mwenye muda mrefu kwenye ligi hiyo, akiwa na miamba ya Anfield kwa miaka minane. Lakini, mwisho wa msimu huu, Mjerumani huyo ataondoka. Jambo hilo linafanya rekodi ya Wenger itadumu kwa miaka mingi na soka la kisasa, itakuwa ngumu kuvunjwa.
18.Mchezaji kuifunga timu moja mfululizo
Rekodi ni mechi 9 na anayeshikilia ni Sadio Mane dhidi ya Crystal Palace. Achana na Luis Saurez dhidi ya Norwich City, lakini kiboko kabisa ni hii ya Mane na Crystal Palace. Suarez amefunga mfululizo dhidi ya Norwich kwenye mechi tano, akifunga mabao 12 ndani ya muda huo, lakini Mane amefunga mfululizo dhidi ya Palace kwenye mechi tisa. Na angeweza kufanya hivyo kwenye mechi ya 10, lakini aliikosa kwa sababu alirudi Senegal kwenye mechi za Afcon 2021.
19. Kufungwa mabao machache ndani ya msimu
Rekodi ni mabao 15 na inashikiliwa na Chelsea katika msimu wa 2004/05. Kuwa na safu ya ulinzi ya mastaa kama Petr Cech, John Terry, Ricardo Carvalho, William Gallas na Paulo Ferreira, kocha Jose Mourinho alitengeneza ukuba wa chuma, ambao ulikuwa haupitiki kirahisi na wapinzani na kuwafanya kwa msimu mzima waruhusu mabao 15 tu kwenye Ligi Kuu England. Hiyo ni rekodi ambayo itachukua muda kuvunjwa kutokana na kasi ya washambuliaji wa sasa na mabeki wepesi wa kizazi kipya.
20. Kufunga bao haraka zaidi akitokea benchi
Rekodi ni sekunde 6 na inashikiliwa na straika Nicklas Bendtner wa Arsenal, aliyefanya hivyo kwenye mechi ya kuwakabili mahasimu wao Tottenham Desemba 22, 2007. Katika mechi hiyo, Bendtner alitokea benchini na ilimchukua sekunde sita tu ndani ya uwanja kufunga bao kwenye North London derby baada ya mpira wa kona. Kufunga kwenye mechi ya mahasimu, ilimfanya Bendtner kuwa shujaa kwa mashabiki wa Arsenal, lakini bao lake la chapchap akitokea benchi, linashikilia rekodi hadi sasa.