Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi zinazibeba Mazembe, Asec CAF

ASEC XMAZEMBE Rekodi zinazibeba Mazembe, Asec CAF

Sun, 7 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya mashabiki wa soka Afrika usiku wa jana kushuhudia shoo kali ya mechi mbili za marudiano za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Yanga na ile ya Al Ahly ya Misri dhidi ya Simba, utamu zaidi unaendelea leo kwa mechi nyingine mbili kupigwa.

Yanga ikiwa ugenini jijini Pretoria iling'olewa kwa penalti 3-2 na Mamelodi baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu kama ilivyokuwa katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa, Kwa Mkapa, huku gumzo likiwa ni bao la Stephane Aziz KI lililokataliwa na VAR pale shuti lake lililotokana na pasi ya Kennedy Musonda kugonga besela na kuangukia ndani.

Simba yenyewe ilikuwa jijini Cairo kurudiana na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo na watetezi wa sasa, Al Ahly na kukumbana na kipigo kingine cha mabao 2-0 baada ya awali kulala 1-0 nyumbani na hivyo kung'olewa kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0.

Hii ni mara ya tano katika misimu sita kwa Simba kutolewa hatua ya robo fainali ikiwamo nne za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuiacha Al Ahly ikienda nusu fainali.

Mamelodi na Al Ahly kwa sasa zinasubiri na kusikilizia matokeo ya mechi zinazopigwa usiku wa leo ili kujua zitakutana na nani katika nusu fainali, huku rekodi zikiwabeba Asec Mimosas ya Ivory Coast na TP Mazembe ya DR Congo dhidi ya wapinzani wao, Petro Atletico ya Angola na Esperance ya Tunisia.

Mazembe iliyolazimishwa suluhu nyumbani wiki iliyopita, itakuwa wageni wa Petro jijini Luanda Angola huku ikiwa na rekodi tamu mbele ya wenyeji wao katka michuano ya CAF.

Katika mechi tatu zilizopita baina ya timu hizo katika michuano hiyo ukiwamo wa wiki iliyopita ulioisha kwa suluhu, Mazembe pia imeshinda mara mbili dhidi ya Petro, ikiifunga nje ndani katika mechi zilizopigwa mwaka 2009. Mazembe ilishinda nyumbani 3-0 na ugenini 2-1 na leo itakuwa na nafasi ya kuendeleza ubabe mbele ya wenyeji ambao inashikilia rekodi kwa msimu huu ikiwa ndio timu pekee ambao wavu wao haujaguswa kabisa hadi sasa.

Ushindi wa aina yoyote kwa Mazembe utaipeleka kuvaana na Al Ahly katika nusu fainali na kukumbushia msimu wa mwaka 2012 zilipokutana makundi na Mazembe kushinda 2-0 baada ya awali kulala 2-1 kwa wababe hao kutoka Misri.

Mashabiki wa soka kuanzia saa 1:00 usiku watapata burudani tamu kutokana na timu zote kucheza soka tamu na la kiufundi, kisha saa 5 usiku watahamia Abidjan, Ivory Coast wakati wenyeji Asec itakapokwaruzana na Esperance ya Tunisia ambao walishindw akufungana katika mechi ya jijini Tunis.

Hilo litakuwa ni pambano la nane baina ya timu hizo kukutana katika michuano ya CAF tangu mwaka 2002, huku Asec ikionekana kuwaburuza wapinzani wao hao, kwani mechi tatu za awali za nyumbani haijawahi kupoteza zaidi ya kushinda tu.

Pia katika mechi nne ilizocheza ugenini ikiwamo ya msimu huu imetoka suluhu mara tatu na mara moja tu ndio iliyopoteza mbele ya Esperance kwa kufungwa mabao 2-0 mwaka 2002.

Kwa rekodi hizo za nyumbani inaipa nafasi kubwa Asec kutoka na ushindi na pengine kutinga nusu fainali kuifuata Mamelodi, ingawa soka huwa lina matokeo ya ajabu, kutokana na ukweli katika mechi ya mkondo wa kwanza Tunis, timu zote zilionyesha soka tamu na la ushindani.

Asec iliyowahi kutwaa taji hilo mara moja msimu wa kwanza tangu kubadilishwa kwa mfumo wa michuano hiyo kutokan Klabu Bingwa Afrika kuwa Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 itakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia Esperance iliyowahi kutwaa taji manne na kushika nafasi ya pili mara nne pia.

Licha ya rekodi ilizonazo Asec inayonolewa na kocha Mfaransa Julien Chevalier, bado timu zote zina nafasi sawa katika mchezo huo utakaoamua mshindi wa kwenda nusu fainali.

Mechi za Mazembe v Petro

2024

TP Mazembe 0-0 Petro Atletico

2009

Petro Atletico 1-2 TP Mazembe

TP Mazembe 3-0 Petro Atletico

Mechi za Asec v Esperance

2024

Esperance 0-0 Asec Mimosas

2007

Asec Mimosas 2-0 Esperance

Esperance 0-0 Asec Mimosas

2005

Asec Mimosas 1-0 Esperance

Esperance 0-0 Asec Mimosas

2002

Asec Mimosas 3-1 Esperance

Esperance 2-0 Asec Mimosas

Chanzo: Mwanaspoti