Kesho Ijumaa, Machi 8, 2024, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Yanga SC, watashuka dimbani kumenyana na Namungo FC kwenye Uwanja wa Majaliwa huko mkoani Lindi.
Yanga SC inatarajia kutua pale Lindi ikiwa ni mara ya 4 kucheza mkoani Lindi dhidi ya vigogo hao wa Ruangwa, Namungo FC.
HISTORIA YA YANGA SC MKOANI LINDI
Kabla ya Yanga SC kucheza Lindi dhidi ya Namungo, mara ya mwisho kucheza Lindi na timu ya Lindi ilikuwa Juni 2, 2002 dhidi ya Kariakoo ya Lindi ambapo mchezo ulitamatika kwa matokeo ya 0-0.
Ukifuatilia historia ya miaka ya nyuma, inasemekana kucheza katika Uwanja wa Ilulu au kucheza Lindi ilionekana kuwa miongoni mwa maeneo magumu sana kupata matokeo mazuri. Lakini haikuwa kazi ngumu sana kwa Yanga SC, ambapo mara kadhaa ilipata matokeo chanya katika uwanja huo.
Mfano mzuri ni msimu wa 2001 ambapo, Kariakoo Lindi hawakupoteza mchezo wowote wakiwa wenyeji, isipokuwa mchezo wa Juni 30, 2001 – Kariakoo 1-3 Yanga SC.
Hapo awali vigogo wengine ambao waliwahi kupata matokeo ya ushindi ni Reli ya Morogoro. Wapinzani wengine aidha hawakwenda uwanjani au mechi zilivunjika katikati ya mchezo.
MCHEZO UJAO NI MCHEZO WA NAMNA GANI?
Mchezo ujao wa Yanga dhidi ya Namungo ni mechi yenye mvuto wa kipekee kutokana na matokeo ya michezo mitatu iliyofanyika Lindi.
Yanga wametoka sare michezo miwili kabla ya kupata ushindi pekee Desemba 7, 2022 ambapo walifanikiwa kupata ushindi wa kwanza Lindi wa magoli 2-0 (Yannick Bangala dk 40, Tuisila Kisinda dk 82).
Kabla ya ushindi huo mara ya mwisho Yanga kushinda mkoani Lindi ilikuwa mwaka 2001.
Takwimu za Yanga SC mkoani Lindi 2000-2020
07/12/2022 – Namungo 0-2 Yanga SC 20/11/2021 – Namungo 1-1 Yanga SC 15/05/2021 – Namungo 0-0 Yanga SC 02/06/2002 – Kariakoo 0-0 Yanga SC 30/06/2001 – Kariakoo 1-3 Yanga SC 2000 – Kariakoo 1-1 Yanga SC 21/04/1999 – Kariakoo 0-0 Yanga SC
Licha ya ugumu katika Uwanja wa Ilulu, tokea mwaka 1998 ambapo Kariakoo walipanda daraja mpaka 2002 waliposhuka, Yanga SC na Reli ndio timu zilizopata ushindi uwanjani ambapo Yanga SC ilipata ushindi mnono wa magoli matatu huko Lindi.