Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi zaibeba Simba kwa KMC

Simba Rekodi X Kmc.jpeg Wachezaji wa Simba wakipasha misuli

Wed, 7 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Achana na kutofanya vizuri katika mechi ya kirafiki, takwimu za kibabe za Simba katika mechi mbili za kwanza, hapana shaka zinawapa kiburi leo wakati watakapoikaribisha KMC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 wakirejea kwenye Ligi Kuu ya NBC baada ya mapumziko ya wiki mbili.

Simba inarejea kwenye Ligi bila Kocha Zoran Maki na wasaidizi wake ambao wameachishwa kazi jana adhuhuri. Inaongoza msimamo wa ligi na pointi zake sita ilizokusanya katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold huku ikifunga mabao matano na kutoruhusu bao lolote.

Na takwimu za udhaifu wa safu ya ulinzi ya KMC ambayo katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu, zinaweza kuiweka Simba katika hali nzuri kisaikolojia ukizingatia makali ya safu yake ya ushambuliaji inayobebwa zaidi na viungo na mawinga wenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao licha ya kutokuwa na mshambuliaji tishio wa kati.

CHAMA VS MATHEO

Wakati KMC wakimchunga zaidi Clatous Chama , wenyeji wanapaswa kuweka jicho la kipekee kiulinzi kwa mshambuliaji Matheo Anthony kutokana na uhatari ambao wachezaji hao kila mmoja ameonyesha katika mechi zilizopita za ligi msimu huu.

Chama ameanza kwa kuonyesha ubora wake uliozoeleka wa kupiga pasi za mwisho na kuchezesha timu ambapo tayari ameshahusika na mabao mawili kati ya matano ya Simba akifunga moja na kupiga pasi moja ya bao. Kwa upande wa Matheo, mabao mawili ambayo yamefungwa na timu hiyo hadi sasa, yamepachikwa na mshambuliaji huyo.

REKODI ZAIBEBA SIMBA

Historia ya mechi nane zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo mbili, inaonyesha kuwa KMC wamekuwa wanyonge mbele ya Simba kwani hawajawahi kupata ushindi au sare hata moja na wamepoteza mara zote nane ambazo wamekutana.

Katika mechi hizo nane, jumla ya mabao 22 yamefungwa ambapo Simba imepachika mabao 18 na mabao manne tu ndiyo yaliyofungwa na watoto wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Ni mechi inayokutanisha idadi kubwa ya wachezaji wanaofahamu vyema kila upande kutokana na kuwahi kuchezea timu hizo kwa nyakati tofauti.

Wakati Simba wakiwa na Israel Mwendwa aliyewahi kuchezea KMC, KMC wao wana Boniface Maganga, David Kisu na Ibrahim Ame waliowahi kuitumikia Simba.

MAKOCHA

Kaimu kocha wa Simba, Selemani Matola alisema; “Tunajua wapenzi na mashabiki wa Simba kuwa mbali na ushindi wanapenda burudani hivyo niwahakikishie kwamba tumejiandaa vizuri na hatutowaangusha.”

“Zile ni mechi za kirafiki na zimeshapita. Kitu kizuri ni kwamba zile mechi zimetupa wigo mpana wa kujua nani ni nani na kuweza kumpa nafasi katika mechi za ligi,” alisema Matola.

Kocha msaidizi wa KMC, Ahmad Ally alisema kuwa wanatambua mchezo utakuwa mgumu kwao lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi.

“Maandalizi kiujumla yapo 90% na hizo 10% tutamalizia uwanjani. Tangu tumesimama ligi angalau kuna kuimarika kwenye timu yetu.”

“Tunakwenda kucheza na timu bora kwa sasa. Tumejaribu kuangalia jinsi ambavyo Simba inacheza na wapi ina uimara na ilipo na udhaifu ili tuweze kupatumia,” alisema Ally.

Chanzo: Mwanaspoti