Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi za kila kocha ni balaa!

Gamondi X Mokwena Rekodi za kila kocha ni balaa!

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga leo usiku kitakuwa uwanjani kumalizana na Azam Fc katika mechi ya Ligi Kuu Bara, kabla ya ligi hiyo kusimama kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, kabla ya benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo kugeukia michezo miwili ya ropbo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga itaikaribisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza itakayopigwa Machi 30 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kisha Aprili 5 zitarudiana Uwanja wa Loftus Versfeld, huko Afrika Kusini na mbabe ataenda nusu fainali kucheza na mshindi kati ya Esperance ya Tunisia na Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Ikiwa zimesalia wiki kama mbili tu kabla ya timu hizo kuvaana kwenye mechi hizo ikiwa ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana katika michuano ya CAF baada ya awali kukutana katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2001 na Wasauzi kushinda kwa matokeo ya jumla ya mabao 6-5, kuna vita nzito kwa makocha wanaozinoa timu hizo.

Yanga inanolewa na Kocha Muargentina, Miguel Gamondi wakati Mamelodi ipo chini ya Rhulani Mokwena na wote kila mmoja anabebwa na rekodi alizonazo ndani ya vikosi hivyo kuanzia michuano ya ndani hadi ile ya kimataifa na pia aina ya mbinu na mifumo inayowabeba kuonyesha mechi zao mbili kutakuwa na kazi kubwa uwanjani.

Ukweli ulivyo ni kwamba makocha hao, kila mmoja ana nafasi kubwa ya kuamua hatma ya timu yake katika hatua ya robo fainali wakati timu hizo zitakapokutana nyumbani na ugenini kutokana na aina ya vikosi ilivyonavyo na pia jinsi zinavyocheza kwa kila upande.

Maandalizi bora kimbinu na mpango mzuri katika mechi hizo mbili baina ya timu hizo sambamba na upangaji sahihi wa vikosi na mabadiliko ya wachezaji siku ya mchezo ni mambo yatakayomuweka kocha mmojawapo katika nafasi nzuri ya kuipeleka timu yake hatua ya nusu fainali na mwingine kukwama.

Yapo baadhi ya mambo ambayo makocha hao wamekuwa wakifanana katika kuyafanyia kazi, lakini wamekuwa wakitofautiana kwa mengine, jambo ambalo linaashiria mechi mbili baina ya timu hizo, zitakuwa na ushindani na mvuto wa aina yake.

MBINU

Mokwena na Gamondi wamekuwa hawafanani katika utumiaji wa mifumo ya kiuchezaji ndani ya uwanja ambapo kila mmoja amekuwa na aina ya mifumo anayoipendelea kuitumia katika kuhakikisha timu yake inapata matokeo mazuri.

Mfumo ambao Gamondi amekuwa akipendelea kuutumia mara kwa mara ni ule wa 4-2-3-1 huku akiwategemea zaidi viungo wa timu hiyo katika kuzalisha na kufunga mabao.

Chini ya Gamondi, Yanga imekuwa ikitegemea soka la kasi linaloambatana na pasi za haraka haraka katika ujenzi wa mashambulizi, ambalo limekuwa mwiba kwa timu pinzani.

Katika aina hiyo ya mfumo, Gamondi ametoa uhuru mkubwa kwa kiungo mmoja anayecheza mbele ya mstari wa ma-beki, kusogea mbele mara kwa mara na kusaidia mashambulizi na jukumu hili mara kwa mara limekuwa likifanywa na Mudathir Yahya, huku kiungo mmoja wa ulinzi akibaki ili kutengeneza balansi na mara nyingi huwa Khalid Aucho.

Mbele yao kunakuwepo na viungo watatu wa ushambuliaji ambao mara kwa mara hucheza kwa kubadilishana nafasi kwa lengo la kuvuruga muundo wa kiulinzi wa timu pinzani na mara kwa mara hukatiza kutokea pembeni kuingia ndani kwa lengo la kuongeza idadi ya wachezaji katika eneo la hatari ili kutengeneza nafasi na kufunga mabao na mara nyingi viungo hao huwa ni Maxi Nzengeli au Augustine Okrah, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.

Ukiondoa mfumo huo wa 4-2-3-1, Gamondi pia hupendelea kutumia mfumo wa 4-4-2.

Kwa upande wa Mokwena, yeye mara nyingi amekuwa akipendelea kutumia mfumo wa 4-3-3 na silaha yake kubwa ni wachezaji wa nafasi za ushambuliaji katika kupika na kufunga mabao.

Kunakuwa na viungo wawili wa ulinzi ambao wanakuwa na jukumu la kuichezesha timu kuanzia nyuma, huku kuki-wepo na kiungo mmoja wa ushambuliaji mwenye jukumu la kuwalisha mipira wachezaji watatu wanaocheza eneo la ushambuliaji.

Viungo hao wawili wa ulinzi mara nyingi huwa ni Teboho Mokoena na Bongani Zungu na anayecheza juu yao huwa ni Marcelo Allende.

Washambuliaji watatu ambao huwa wanatumika sana na Mokwena ni Peter Shalulile, Themba Zwane na Thembinkosi ‘Nyoso’ Lorch.

Mokwena pia hupendelea kutumia mfumo wa 3-4-3.

UBABE KATIKA LIGI

Makocha hao kila mmoja ameonekana kuwa tishio kwenye ligi ya nchi yake na wote wako kwenye nafasi nzuri ya kuziongoza timu zao kutwaa ubingwa katika ligi zao.

Kwa hapa Tanzania, Gamondi ameiwezesha Yanga kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imekusanya pointi 52 katika mechi 19 ilizocheza ambapo sasa inahitaji ushindi katika mechi nane kati ya 11 zilizobakia ili iweze kutwaa ubingwa, huku ikifunga mabao 48 na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa. Kwa ujumla katika Ligi Kuu, Yanga imeshinda mechi 17, kutoka sare moja na kupoteza pia moja.

Mamelodi katika Ligi ya Afrika Kusini, inaongoza ikiwa na pointi 46 ilizovuna katika mechi 18, ikihitaji ushindi katika mechi sita tu ili iweze kutwaa ubingwa kwa msimu wa saba mfululizo.

Wakati Yanga ikipoteza mechi moja tu ya ligi, Mamelodi Sundowns yenyewe haijapoteza mechi yoyote hadi sasa kati-ka ligi hiyo ya Sauzi maarufu kama (PSL), kwani imeshinda mechi 14 na kutoka sare nne, ikifunga mabao 33 na kufungwa matano. Hii inaonyesha timu hizo hazitofautiani sana kwenye anga hizo, japo Yanga inaonekana kuwa wa-kali zaidi kwa kukusanya alama nyingi licha ya kupoteza mechi moja na safu yake inafunga mabao mengi.

KIMATAIFA USIPIME

Timu hizo zinakutana kila moja ikiwa haina takwimu za kinyonge kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo am-bayo Mamelodi katika mechi sita ilizocheza katika Kundi A, imeshinda nne, kutoka sare moja na kupoteza moja, iki-funga mabao saba na kufungwa moja, wakati Yanga iliyokuwa Kundi D, imeshinda mechi mbili, sare mbili na kupote-za pia mbili, ikifunga mabao tisa na kufungwa sita.

Ukiangalia kwenye michuano ya CAF, licha ya Yanga kuwa kiwembe eneo la mbele kuliko Mamelodi, lakini imekuwa na ukuta mwepesi tofauti na wenzao, hivyo kufanya kwenye mechi zao kuwepo kwa vita nzito kati ya safu za ulinzi na ushambuliaji za timu hizo ili kuhakikisha mambo yanakuwa mepesi na kufuzu nusu fainali.

Hata hivyo, kwa namna Mamelodi ilivyo bora kwa miaka ya karibuni hasa anga hizo za kimataifa ni wazi Yanga hai-paswi kubweteka kwa takwimu ilizonazo badala yake ifunge mkanda ili iepuke kunyweshwa kikombe cha uchungu itakapokutana na timu hiyo maarufu kama Masandawana a.k.a The Brazilians.

VIKOSI

Timu zote zina vikosi bora vyenye wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kusakata soka ambao katika mechi za hatua za awali hadi makubwa wamefanya kazi kubwa zilizowabeba makocha wa timu hizo ambao safari wanaenda kuamua mmoja aende nusu fainali na mwingine arudi nyumbani.

Pacome Zouzoua anayeongoza kwa mabao kwa Yanga akifunga matatu na kuasisti moja ndiye tishio kwa Mokwena, mbali na uwepo wa Stephane Aziz KI, Maxi Nzengeli, Augustine Okrah, Mudathir Yahya, Kennedy Musonda na kipa Diarra Djigui wenye uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa ndio silaha ya Yanga mbele ya Mamelodi.

Kwa upande wa Mamelodi silaha kuu ni Peter Shalulile mwenye mabao mawili na asisti moja, lakini ina wakali wen-gine wasiotabirika akiwamo nahodha, Teboho Mokoena, Lucas Ribeiro Costa, Themba Zwane na kipa Ronwen Wil-liams ambaye amekuwa mahiri akiibeba Masandawana hadi timu ya taifa ya Afrika Kusini iliyomaliza ya tatu Afcon 2023.

Makocha hao kwa sasa wanakuna vichwa juu ya namna gani watakavyokabiliana, lakini wakiombea silaha zote ziwe salama hadi siku ya mechi hizo dakika 180 ziamue mbabe baina yao kwa mmoja kupigwa na kuing’oka michuanoni.

WASIKIE WADAU

Kocha wa Dodoma Jiji, Mkenya Francis Baraza alisema kuwa kinachohitajika ni Gamondi kufanya maandalizi mazuri ya kimbinu na kisaikolojia kwa wachezaji wake.

“Mamelodi Sundowns ni timu nzuri lakini sio kwamba haifungiki. Ukiitazama Yanga ina kikosi kizuri cha kuweza kupambana nao na kupata matokeo mazuri kama itajiandaa vizuri kwenye mbinu na kujenga hali ya kujiamini kwa wachezaji,” alisema Baraza.

Nyota wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars aliyewahi kucheza soka la kulipwa Angola, Said Maulid ‘SMG’ alisema kuwa ana imani kubwa kuwa timun yake itaitupa nje ya mashindano Mamelodi Sundowns.

“Yanga hivi sasa ina kikosi bora ambacho kina uwezo wa kucheza na timu nyingine yoyote Afrika na nina imani kubwa na kocha Gamondi,” alisema SMG aliyesifika enzi zake kwa kasi, chenga na kuwatungua makipa akicheza kama winga.

Chanzo: Mwanaspoti