Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi za kibabe Real Madrid ikibeba ndoo Ulaya tena

Real Madrid Uefaaaaaaaaaa Rekodi za kibabe Real Madrid ikibeba ndoo Ulaya tena

Sun, 2 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Real Madrid imeendeleza ubabe wake katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikithibitisha hakuna wa kuikaribia baada ya kutwaa taji hilo kwa mara ya 15 kwa kuifunga Borussia Dortmund 2-0 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Wembley, London.

Kuna rekodi kadhaa za kibabe zimeweka katika mechi hii ikiwamo ya Real Madrid sasa kuwa imelitwaa taji hilo zaidi ya mara mbili ya wapinzani wao wa karibu.

15 - Real Madrid imeshinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambalo zamani lilijulikana kama European Cup kwa mara ya 15 katika historia yao, mataji ambayo ni zaidi ya mara mbili ya timu nyingine yoyote (AC Milan ndio inafuatia kwa kulitwaa mara 7).

6 - Toni Kroos sasa ameshinda mataji sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na katika historia ya michuano hiyo, hakuna mchezaji aliyeshinda tajio hilo mara nyingi zaidi yake. Lakini amelingana na Paco Gento, Nacho Fernandez, Luka Modric na Dani Carvajal ambao pia wameshinda taji hilo mara sita kila mmoja. Kroos alitangaza kwamba hiyo ndio mechi yake ya mwisho kucheza soka na kwamba anastaafu kwa sababu hataki kuchezea klabu nyingine baada ya Real Madrid.

22 - Vinicius Junior amehusika moja kwa moja katika mabao 22 katika mechi za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya (kafunga mabao 11, katoa asisti 11); idadi ambayo ni ya juu zaidi kwa mchezaji ambaye hajafikisha umri wa miaka 24, akiifikia rekodi ya Lionel Messi.

8 - Vinicius Junior alipiga chenga 8 kimafanikio dhidi ya Borussia Dortmund, idadi ambayo ni sawa na jumla ya chenga walizopiga wachezaji wengine wote ukiwajumuisha pamoja waliocheza mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa jana (8). Kiufupi, hiyo ni idadi kubwa zaidi ya mchezaji mmoja kuwatoka wapinzani katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu Lionel Messi mwaka 2015 aliposepa na kijiji mara 10 katika mechi dhidi ya Juventus. Barcelona ilishinda fainali hiyo kwa mabao 3-1 yaliyofungwa na Ivan Rakitic, Luis Suarez na Neymar, huku la Juve likiwekwa na Alvaro Morata.

1 - Kukutana uwanjani kwa Jadon Sancho wa Borussia Dortmund na Jude Bellingham wa Real Madrid, hii ni mara ya kwanza kwa wachezaji raia wa Uingereza kukutana katika mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu imeanzishwa huku wote wakizitumikia klabu ambazo sio za kutoka England.

0 - Thibaut Courtois amecheza fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya bila ya kuruhusu bao akiitumikia Real Madrid (dhidi ya Liverpool mwaka 2022 na dhidi ya Borussia Dortmund 2024).

Takwimu zake katika mechi hizo:

Amepigiwa mashuti (12)

Ameokoa (12)

Mabao aliyofungwa (0)

2 – Mashuti mawili ambayo Real Madrid ilipiga dhidi ya Borussia Dortmund katika kipindi cha kwanza ndio machache zaidi kwa timu hiyo kupiga katika kipindi cha kwanza kwenye michuano yote msimu huu.

Chanzo: Mwanaspoti