Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi za Simba, Yanga Ngao ya Jamii

Rekodiiiiiiiiiii Rekodi za Simba, Yanga Ngao ya Jamii

Thu, 8 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia na rekodi za timu hizi. Kwa upande wa mashabiki, hii ni fursa ya kuona mchezo wa kuvutia na kila timu itajitahidi kwa nguvu zote kuhakikisha inamzidi mwenzake.

Rekodi zinaonyesha, tangu mwaka 2001 zilipoanza kuchezwa mechi za Ngao ya Jamii, Simba inaongoza kubeba taji hilo mara nyingi , 10, inafuatiwa na Yanga mara saba, kisha Mtibwa Sugar na Azam zilizochukua mara moja, Mbali na hapo, hakuna timu nyingine iliyowahi kushinda Ngao ya Jamii.

Katika mechi hizo za nusu fainali ya Ngao ya Jamii, hapa kuna uchambuzi wake na rekodi kadhaa zilizowekwa huko nyuma na kinachotarajiwa kutokea mwaka huu.

REKODI ZA ZAMANI

Mpaka sasa zimechezwa fainali 19 za Ngao ya Jamii kuanzia 2001, huku ikionyesha mwaka 2004, 2006, 2007 na 2008 haikuchezwa, ikaendelea 2009 hadi sasa.

Mara ya kwanza zinaanza kuchezwa mechi hizo, Yanga iliichapa Simba mabao 2-1, wafungaji wa Yanga ni Edibily Lunyamila na Ally Yusuph 'Tigana' huku la Simba likifungwa na Steven Mapunda 'Garincha'.

Mara ya mwisho mwaka jana Simba iliifunga Yanga 3-1 kwa penalti baada ya dakika tisini matokeo kuwa 0-0.

Simba na Yanga katika Ngao ya Jamii zimekutana mara tisa huku rekodi zikionyesha Simba imeshinda mechi tano na Yanga ikishinda nne.

Yanga inakumbuka misimu mitatu nyuma iliifunga Simba mara mbili mfululizo 2021 na 2022 kabla ya Simba kulipa kisasi mwaka 2023.

Mchezo huu wa Simba dhidi ya Yanga utakuwa ni wa nne mfululizo tangu 2021, hivyo ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa ikizingatiwa katika Kipindi hicho Yanga imeshinda mbili na Simba moja, safari hii itataka kushinda ili kuweka mzani sawa kwenye mambo mawili.

Kwanza kubeba taji lao la 11 la Ngao ya Jamii na kuikimbia zaidi Yanga, kisha kushinda ili nayo iwe imeshinda mara mbili katika nne walizokutana hivi karibuni ndani ya michuano hiyo.

Yanga yenyewe inataka kuendeleza ubabe mbele ya Simba kwani tangu mara ya mwisho ipoteze katika Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao hao, wakaja kushinda mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara 2023-2024 tena kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-2. Ile ya kwanza ilikuwa Simba 1-5 Yanga kisha Yanga 2-1 Simba.

USHINDANI SASA

Ukiangalia vikosi vya timu zote mbili vina mabadiliko ya wachezaji, lakini Simba ndiyo ina maingizo mapya mengi ambayo yamefika 14, wakati Yanga wachezaji wapya ni saba.

Majembe mapya ya Simba yanayotarajiwa kuibeba timu hiyo ni raia wa kigeni wanane ambao ni Valentin Nouma, Chamou Karabou, Charles Ahoua, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Steven Mukwala na Moussa Camara.

Wazawa ni Kelvin Kijiri, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Awesu Awesu, Omary Omary na Valentino Mashaka. Lameck Lawi alikuwa wa kwanza kutambulishwa lakini usajili wake umezua utata, hata hivyo hayupo kambini na ametimkia Ulaya.

Wachezaji saba wapya wa Yanga ni Khomeny Abubakari, Chedrack Boka, Clatous Chama, Aziz Andabwile, Duke Abuya, Prince Dube na Jean Baleke. Wazawa wawili pekee kwenye listi hiyo Khomeny na Andabwile.

Usajili wa pande mbili kwa timu hizo ndiyo unaufanya mchezo huu kusubiriwa kwa hamu kwani Simba inaamini imeimarisha kikosi chao wakati Yanga ikitamba imefanya maboresho kidogo tu yanayoweza kuwapa tena furaha.

Simba na Yanga mwaka huu kwao itakuwa ni mara ya 15 kushiriki Ngao ya Jamii. Simba ikiwa imeshinda Ngao ya Jamii 10, imepoteza nne, wakati Yanga imeshinda saba na kupoteza saba.

Wakati ratiba inapangwa na kuonyesha Yanga itacheza dhidi ya Simba, Kocha Mkuu wa Yanga, Gamondi alisema, "Mchezo wa juzi ulikuwa maalum kwa kuwafurahisha mashabiki wetu ambao wamefanya kitu kikubwa kwenye siku yao kubwa."

Hata hivyo, Gamondi aliongeza kuwa furaha ya mechi hiyo sasa imepita na wanahitaji kuanza maandalizi kwa ajili ya mchezo ujao wa Derby.

"Sasa tunaanza hesabu mpya kwa ajili ya mchezo wa Derby. Nilijaribu kuwaangalia Simba na nimeona wamefanya usajili mzuri na kwa jumla wana timu nzuri.

Hata hivyo, nataka kuwakumbusha wachezaji wetu waachane na picha ya wapinzani wetu kama ilivyokuwa msimu uliopita," alisema Gamondi.

Wakati Gamondi wakati anaanza kuinoa Yanga msimu uliopita, alishindwa kutetea Ngao ya Jamii iliyobebwa na Simba, safari hii Fadlu ana kazi ya kulitetea taji hilo Simba ililobeba msimu uliopita.

Huu utakuwa ni mtihani wa kwanza kwa Kocha Fadlu Davids ambaye anainoa Simba akichukua mikoba ya Abdelhak Benchikha.

Fadlu amesema: “Kucheza dhidi ya Yanga ni sehemu ya mchezo tu kama michezo mingine, ni mchezo mkubwa na naamini utakuwa mzuri upande wetu na kuondoka na ushindi. Tunataka kuona tunaanza vizuri.”

Mchezo huu utatoa picha ya hali halisi ya timu hizi na jinsi zinavyokabiliana na changamoto za msimu mpya.

Chanzo: Mwanaspoti