Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi za Robertinho tangu atue Simba zinatisha

Robertinho Mtego.jpeg Rekodi za Robertinho tangu atue Simba zinatisha

Tue, 26 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba imefikisha jumla ya mechi 25 ikiwa chini ya kocha Roberto Oliveira 'Robertinho', huku kocha huyo raia wa Brazil akiwa na rekodi zake tofauti zinazombeba ndani ya timu hiyo.

Kwenye idadi hiyo ya michezo ya Simba Robertinho ameweka rekodi ya kuiongoza Simba kucheza mechi 14 za Ligi Kuu Tanzania Bara na hadi sasa hajapoteza mechi yoyote si nyumbani wala ugenini.

Robertinho, ambaye mchezo wake wa kwanza wa ligi ulikuwa Januari 18, 2023 alipoiongoza Simba kushinda nyumbani kwa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City, msimu uliopita aliiongoza Simba kucheza mechi 11 bila kupoteza.

Simba ilishinda mechi tisa kati ya 11, ikizifunga Mbeya City (3-2), Dodoma Jiji (0-1), Singida Big Stars (3-1), Mtibwa Sugar (0-3), Ihefu (0-2), Yanga (0-2), Ruvu Shooting (0-3), Polisi Tanzania (1-6), kisha ikamalizia msimu kwa kuichapa Coastal Union (3-0), huku ikitoa sare mbili pekee dhidi ya Azam FC (1-1) na ile na Namungo (1-1)

Avuna Ngao ya Jamii

Msimu huu, Robertinho ameanza na 'zali' akifanikiwa kuipa Simba taji la kwanza ikiwa chini yake alipoiongoza Simba kutwaa Ngao ya Jamii akiwavua watani wake, Yanga kwa matuta katika fainali iliyofanyika jijini Tanga na katika mechi mbili alizocheza alifanikiwa kufuzu zote kwa njia ya mikwaju ya penalti.

Msimu huu bado yumo

Robertinho ndani ya msimu huu bado yuko kwenye ubora wake akiwaongoza Simba kushinda mechi zote tatu za kwanza akianza na Mtibwa Sugar (2-3), Dodoma Jiji (2-0) kisha juzi ikapata ushindi mkubwa mbele ya Coastal Union wa mabao (3-0).

Katika misimu miwili iliyopita, Simba haikuwahi kushinda mechi zote, kwani msimu wa juzi alitoka suluhu na Biashara United na uliopita akianza kwa sare na KMC.

Pia, huu ni msimu pekee kwa Simba kuwa na mchezaji mwenye mabao matano kwenye mechi tatu na 'hat-trick' moja, licha ya mashabiki kusisitiza kuwa bado timu yao haina kiwango ilichokitarajia uwanjani.

Kimataifa mzani sawa

Mechi za kimataifa kuanzia msimu uliopita, Robertinho ameiongoza Simba kwenye mechi nane na kati ya hizo Wekundu wa Msimbazi walishinda nne dhidi ya Vipers (0-1) ugenini kisha kupata matokeo kama hayo nyumbani.

Akawachapa Horoya AC (7-0) mechi zote zikiwa za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kwenye hatua ya robo fainali akitangulia kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Wydad Athletic.

Akapoteza pia michezo minne alipofungwa na Horoya AC (1-0), Raja Athletic nyumbani na ugenini, kisha akapoteza mchezo wa marudiano wa robo fainali kwa bao 1-0, kisha Simba kung'olewa kwa matuta.

CAF aanza na sare

Msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Robertinho alianza kwa kulazimisha sare ugenini ya mabao 2-2 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia ikiwa ni mechi ya mtoano na timu hizo zitarudiana wikiendi hii hapa nchini kuamua timu ipi itatinga hatua ya makundi.

Wadau watoa yao

Kocha na beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa akizungumzia mwenendo huo wa Robertinho ndani ya klabu hiyo, alisema bado hajaona kama kocha huyo amepoteza mwelekeo licha ya mashabiki kuonekana kumpa presha akiwataka kuanza kuelewa falsafa ya Mbrazil huyo.

"Robertinho yuko kwenye njia sahihi, ukiangalia anavyokwenda hadi sasa, kitu pekee ambacho nakiona hajikaeleweka kwa mashabiki wa Simba hawajajua falsafa ya Robertinho ni ipi, wakishaelewa watanyamaza," alisema Pawasa.

"Tangu anafika hapa alisema (Robertinho) anataka kuona Simba inacheza soka la kushambulia na kupiga pasi za kwenda mbele sasa mashabiki wao wanasahau kwamba msimu huu Robertinho ana timu karibu mpya ambayo inahitaji muda kidogo kuweza kuwaunganisha wachezaji hawa wapya waliokuja na wale waliokuwepo bila kuharibu msingi wa timu.

"Simba ilisajili wachezaji wengi eneo la kiungo ambalo ndio roho yao ya timu na hapohapo wakafanya usajili wa wachezaji wengi wa eneo hilo, hatua hii inamfanya kocha kuhitaji muda.

"Kitu ambacho naweza kumshauri Robertinho anatakiwa kuzungumza na kocha wake wa mazoezi naiona Simba bado haijaweza kuwa sawa kimazoezi, kiwango cha ufiti wa miili ya wachezaji bado sio kikubwa kama ambavyo tunaziona klabu zingine kama Yanga ambao ndio wanaonekana wameiva vuzuri."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: