Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi ya Kagere yageuka kaa la moto

Meddie Kagere Rec Rekodi ya Kagere yageuka kaa la moto

Sun, 19 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere kwa sasa anaichezea Namungo ila wakati anaondoka Msimbazi, nyota huyo raia wa Rwanda aliweka rekodi tamu kwa mastaa wa kigeni katika Ligi Kuu Bara ambayo hata yeye ameshindwa kuifikia.

Kagere alitua Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-2019 na kufunga jumla ya mabao 23 na kuipiku rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ya wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi msimu mmoja alipofunga 21 msimu wa 2015-2016.

Msimu wa pili kwa staa huyo akiwa na Simba pia, alifunga mabao 22 na kutetea Tuzo ya Mfungaji Bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo hiyo mara mbili mfululizo.

Rekodi hiyo ya Kagere ya kuibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo inaendelea kuwatesa washambuliaji kwa sababu hadi sasa licha ya kasi kubwa ya ufungaji kwa mastaa mbalimbali ila inaonekana ni ngumu kuifikia kutokana na hali ilivyo.

Msimu uliopita Tuzo ya Mfungaji Bora ilienda kwa Fiston Mayele aliyekuwa Yanga na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ aliyeanza kuichezea Geita Gold kisha kujiunga na Simba dirisha dogo na kila mmoja alifunga mabao 17.

Rekodi hiyo inaonekana ni ngumu kufikiwa na Saido msimu huu kwani hadi sasa amefunga mabao saba tu akiwa na Simba, huku Mayele akiondoka Yanga baada ya kupata dili nono la kujiunga na matajiri wa Misri, klabu ya Pyramids.

Msimu huu vita kali ipo kwa mastaa wawili ambao ni Stephane Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC ambao kila mmoja hadi sasa amefunga mabao 15 ya Ligi Kuu Bara huku ikibakia michezo mitatu kwa kila timu msimu kutamatika.

Akizungumzia rekodi hiyo inayoendelea kuwatesa washambuliaji hadi sasa, Kagere alisema, suala hilo hutokea kwa bahati tu kwa sababu Ligi ya Tanzania ni ngumu kuchezea na kadri unavyozidi kuonyesha ubora ndivyo unavyozidi kukamiwa.

“Kwangu ni jambo la kujivunia, ila siku zote huwa napenda kuwapongeza wachezaji wenzangu ambao nimekuwa nikicheza nao, kwa sababu tumekuwa tukishirikiana, hivyo kunirahisishia majukumu yangu,” alisema Kagere mwenye mabao mawili msimu huu.

Chanzo: Mwanaspoti