Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi ya Fergie hatarini kuvunjwa

Alex F Gwiji wa Manchester United, Sir Alex Ferguson

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Gwiji wa Manchester United, Sir Alex Ferguson yupo kwenye hatari ya kupoteza rekodi yake tamu ya Ligi Kuu England ambayo imedumu kwa miaka 11.

Kocha huyo mashuhuri aliweka rekodi hiyo katika msimu wa 2012/13, ambao ndiyo ulikuwa wa mwisho kwa Man United kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.

Katika msimu huo, ambapo aliipa Man Unitd taji la 13 la Ligi Kuu England, Ferguson alishuhudia kikosi chake kikiwa na wafungaji 20 tofauti kwenye mechi za ligi.

Hakuna timu nyingine kwenye historia ya Ligi Kuu England, ambayo iliweka rekodi ya kuwa na wafungaji 20 tofauti ndani ya msimu mmoja wa ligi, huku ikiwa na mastaa kama Robin van Persie na Wayne Rooney, Man United ilitikisa nyavu za wapinzani wao mara 86.

Na sasa miaka 11, rekodi hiyo bado imesimama. Hata hivyo, kuna hatari ya kuvunjwa mwaka huu na wanaokaribia kufanya hivyo ni Newcastle United.

Kikosi hicho cha kocha Eddie Howe kimekuwa vizuri, ambapo hadi sasa kwenye ligi, tayari kimeshashuhudia wafungaji 19 tofauti kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Newcastle imefunga mabao 57 msimu huu, huku mabao hayo yakifungwa na wachezaji 19 tofauti, mchezaji mmoja tu kufikia maajabu ya Ferguson.

Hivyo, akipatikana mfungaji mmoja tofauti wikiendi hii watafikia rekodi hiyo ya Ferguson na kama watapatikana wawili tofauti, basi watakuwa wamevunja na kuandika rekodi mpya. Wataweza? Mastaa wa Newcastle United ambao hawajafunga hadi sasa ni Lewis Hall, Matt Targett, Emil Krath na Elliot Anderson, wakiungana na makipa wao Nick Pope, Martin Dubravka na Loris Karius.

Newcastle bado ina mechi 11 zimebaki kwenye ligi, hivyo inaweza kutengeneza historia na kuvunja rekodi hiyo ya Ferguson iliyodumu kwa miaka 11 kwenye Ligi Kuu England.

WAFUNGAJI WA MAN UNITED 2012/13

-Robin van Persie: 26, Wayne Rooney: 12, Javier Hernandez: 10, Shinji Kagawa: 6, Patrice Evra: 4, Rafael: 3, Jonny Evans: 3, Tom Cleverley: 2, Alex Buttner: 2, Ryan Giggs: 2, Nick Powell: 1, Antonio Valencia: 1, Paul Scholes: 1, Anderson: 1, Rio Ferdinand: 1, Darren Fletcher: 1, Nemanja Vidic: 1, Nani: 1, Michael Carrick: 1, Danny Welbeck: 1.

WAFUNGAJI WA NEWCASTLE 2023/24

-Alexander Isak: 11, Anthony Gordon: 9, Callum Wilson: 7, Sean Longstaff: 4, Fabian Schar: 3, Miguel Almiron: 3, Bruno Guimaraes: 3, Dan Burn: 2, Sven Botman: 2, Joelinton: 2, Harvey Barnes: 2, Kieran Trippier: 1, Tino Livramento: 1, Lewis Miley: 1, Jamaal Lascelles: 1, Jacob Murphy: 1, Sandro Tonali: 1, Matt Ritchie: 1, Joe Willock: 1.

Chanzo: Mwanaspoti