Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi tamu kinoma kwenye Ligi Kuu England

Haaland Hat Trick Erling Haaland

Wed, 25 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Supastaa, Erling Haaland amefunga hat-trick tatu kwenye mechi nane alizocheza kwenye Ligi Kuu England, akivunja rekodi ya mkali Michael Owen, ambaye alihitaji mechi 48 kufikisha idadi hiyo ya hat-trick tatu.

Kwenye Ligi Kuu England kuna rekodi nyingi tamu zinazobamba, lakini hizi hapa 19 bado hazijavunjwa na huenda zikadumu muda mrefu kutokana na upekee wake.

1. Kufunga hat-trick tatu kwenye mechi chache (Mechi 8 - Erling Haaland - 2022/23)

Hii ni rekodi ya hivi karibuni. Erling Haaland aliwasili England majira ya kiangazi 2022 na hakutaka muda mrefu, kwani ndani ya mechi nane tu alizocheza Ligi Kuu England, tayari amefunga hat-trick tatu dhidi ya Aston Villa, Wolves na Man United.

2. Mechi nyingi bila ya kupoteza (Mechi 49 – Arsenal – Mei 7, 2003 hadi Oktoba 24, 2004)

Ni Arsenal pekee ambayo ilicheza kwa msimu mzima wa Ligi Kuu England bila ya kupoteza mechi. Hakuna timu nyingine imewahi kufanya hivyo. Na Arsenal inashikilia rekodi nyingine tamu ya kucheza mechi nyingi bila ya kupoteza kwenye Ligi Kuu England. Mechi 49.

3. Kucheza mechi mfululizo (Mechi 310 – Brad Friedel – Agosti 14, 2004 hadi Septemba 29, 2012)

Kwa vikosi vipana na mfumo wa kisasa, haiwezekani kwa mchezaji mmoja kucheza mfululizo kwenye mechi 310. Rekodi hiyo kwenye Ligi Kuu England inashikwa na kipa Brad Friedel, ambaye alipita kwenye timu za Blackburn Rovers, Aston Villa na Tottenham.

4. Pointi chache zaidi kwenye msimu (Pointi 11 – Derby County 2007/08)

Derby inasali kila siku kuomba itokee kwenye Ligi Kuu England timu itakayovuna pointi chache zaidi ya 11 ilizovuna. Lakini, rekodi hiyo hadi sasa bado haijavunjwa. Hata Sunderland kwenye msimu wake wa hovyo 2005/06, ilivuna pointi 15.

5. Vichapo vingi mfululizo (Vichapo 20 - Sunderland - 2003 hadi 2005)

Sunderland ndiyo timu iliyopita kwenye kipindi kigumu zaidi katika historia ya Ligi Kuu England. Timu hiyo ilikula vichapo 20 mfululizo. Ilipoteza mechi 15 msimu wa 2002/03, ikashuka daraja. Ilipopanda tena, ikachapwa tano za kwanza mfulilizo.

6. Mchezaji mwenye umri mkubwa (John Burridge – miaka 43 na siku 162 - Man City vs QPR, Mei 14, 1995)

Ipo wazi, John Burridge alikuwa kipa na kuweka rekodi hiyo ya kucheza mechi ya Ligi Kuu England akiwa na umri mkubwa zaidi, miaka 43 na siku 162. Teddy Sheringham anashikilia rekodi ya mchezaji wa ndani, miaka 40 na siku 272 aliyoweka akiwa West Ham, Desemba 2006.

7. Tofauti ndogo ya pointi za bingwa (Pointi 0, mabao 8 - Man City 2011/12)

Unakumbuka hii “AGUUUERRRROOOOOO.” Hiyo ni sauti ya mtangazaji alipotangaza bao la Sergio Aguero akiifungia Manchester City bao ambalo liliipa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kuizidi Manchester United kwa tofauti ya mabao manane tu baada ya kulingana pointi.

8. Bao la haraka zaidi (Sekunde 7.69 – Shane Long vs Watford, Aprili 23, 2019)

Ilionekana kama haiwezekani hivi bao kufungwa kwa haraka sekunde saba tu kwenye Ligi Kuu England, lakini hilo alilifanya straika Shane Long kipindi anaitumikia Southampton, ambapo alifunga dhidi ya Watford kwenye sekunde ya saba tu ya mchezo baada ya kuanza.

9. Pointi chache zilizoshinda ubingwa wa ligi (Pointi 75 – Man United 1996/97)

Wakati Manchester City na Liverpool zikikaribia pointi 100 karibu katika kila msimu miaka ya karibuni, hebu fikiria kuna timu ilibeba ubingwa wa ligi ikiwa na pointi 75. Hiyo ilifanya Manchester United msimu wa 1996/97. Hakuna bingwa mwingine wa pointi chache.

10. Mechi nyingi bila ya kupoteza nyumbani (Chelsea, mechi 86 – Machi 20, 2004 hadi Oktoba 5, 2008)

Mechi 86 nyumbani bila ya kupoteza. Hiyo ni rekodi ya kibabe kabisa iliyowahi kuwekwa na Chelsea. Liverpool walijaribu kuifukuzia, lakini walishindwa zikiwa zimebaki mechi 17 mbele yao kufikia rekodi hiyo, wakachapwa nyumbani kwenye mikikimikiki ya ligi.

11. Mahudhurio hafifu zaidi kwenye mechi (Mashabiki 3,039 - Wimbledon vs Everton, Januari 26, 1993)

Katika kipindi kisichokuwa cha Uviko 19, mechi ya Wimbledon na Everton ndiyo iliyoweka rekodi ya kuingiza mashabiki wachache zaidi kwenye Ligi Kuu England. Mechi hiyo ilichezwa uwanjani Selhurst Park ilivutia mshabiki 3,039 huku 1,500 walikuwa wa Everton.

12. Hat-trick ya haraka (Dakika 2, sekunde 56– Sadio Mane vs Aston Villa, Mei 16, 2015)

Erling Haaland anaweza kuwa mfalme wa hat-trick, lakini bado hajavunja rekodi ya Sadio Mane aliyoweka akiwa Southampton, alipofunga hat-trick ya haraka, alipotumia dakika 2 na sekunde 56 tu, kutikisa mara tatu nyavu za Aston Villa. Rekodi hiyo bado haijavunjwa.

13. Kucheza muda mrefu bila kuruhusu bao (Edwin van der Sar (Man United, dakika 1,113)

Kipa Edwin van der Sar aliweka rekodi ya kucheza muda mrefu bila ya kuruhusu bao, dakika 1,113 kuanzia Novemba 15, 2008 hadi Februari 18, 2009. Msimu wa 2008/09, Van der Sar alicheza mechi 14 mfululizo bila kufungwa hadi hapo Roque Santa Cruz alipovunja rekodi.

14. Kufunga kwenye misimu mfululizo (Ryan Giggs – misimu 21, 1992/93 hadi 2012/13)

Kucheza kwenye Ligi Kuu England kwa misimu 21 si jambo dogo. Na hilo lilifanywa na mkali Ryan Giggs, ambaye si kwamba alicheza tu, bali alifunga bao katika kila msimu. Kwa kifupi Giggs alifunga kwenye misimu 23, lakini miwili ya kwanza EPL ilikuwa haijaanza.

15. aliyefunga mabao mengi kipindi kimoja (Jermain Defoe - mabao 5, Tottenham vs Wigan, Novemba 22, 2009)

Hii ni rekodi inayosikiliziwa kama Erling Haaland ataweza kuivunja. Kuna wachezaji watano waliowahi kufunga mara tano kwenye mechi moja ya Ligi Kuu England, lakini staa Jermain Defoe aliweka rekodi ya kufunga mara tano kipindi kimoja. Spurs ilishinda 9-1.

16. Kocha aliyedumu timu moja miaka mingi (Miaka 21, siku 224 – Arsene Wenger, Arsenal)

Kocha, Arsene Wenger alitua Arsenal Oktoba Mosi, 1996 na kudumu hapo hadi Mei 13, 2018 alipoondoka, karibu miaka 22. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp kwa sasa ndiye aliyedumu siku nyingi kwa waliopo kwenye Ligi Kuu England, miaka minane.

17. Kufunga mfululizo dhidi ya timu moja (Sadio Mane- mara 9 vs Crystal Palace)

Luis Saurez ameitesa sana Norwich City, lakini Sadio Mane akiwa Liverpool aliweka rekodi ya kuifunga Crystal Palace mara tisa mfululizo kwenye Ligi Kuu England. Suarez aliifunga Norwich kwenye mechi tano mfululizo, lakini Mane mara tisa mfululizo dhidi ya Palace.

18. Kufungwa mabao machache kwa msimu (Chelsea, mabao 15 – 2004/05)

Ikiwa na Petr Cech golini na ukuta wa mabeki John Terry, Ricardo Carvalho, William Gallas na Paulo Ferreira, Chelsea ya Jose Mourinho ilikuwa haifungiki kirahisi msimu wa 2004/05. Kwa msimu mzima, kwenye Ligi Kuu England iliruhusu mabao 15 tu.

19. Bao la haraka kutokea benchi (Sekunde ya 6 – Nicklas Bendtner, Arsenal vs Tottenham, Desemba 22, 2007)

Hakuna bao tamu kama kuingia tu uwanjani na ndani ya muda mfupi unaifungia timu yako. Hilo alilifanya Nicklas Bendtner, alitumia sekunde sita tu kufunga kwenye North London derby, Arsenal dhidi ya Tottenham.

Chanzo: Mwanaspoti