Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi sita zinasakwa nusu fainali Shirikisho

Rekodi Sitaaa Rekodi sita zinasakwa nusu fainali Shirikisho

Sat, 18 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mechi za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) zikichezwa leo na kesho jijini Mwanza na Arusha, rekodi sita tofauti zinazoweza kuwekwa au kufikiwa au kushindikana kuvunjwa kutokana na matokeo yatakayopatikana.

Nusu fainali ya kwanza itachezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo kuanzia saa 9:30 alasiri baina ya Azam na Coastal Union na mchezo mwingine wa nusu fainali utakuwa kesho kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha kuanzia saa 9:30 alasiri.

Rekodi inayosubiriwa kwa hamu kuona kama inaweza kuvunjwa au la ni ile ya idadi kubwa ya mabao kuwahi kufungwa katika mechi za nusu fainali ya mashindano hayo ambapo hadi sasa msimu uliozalisha idadi kubwa ya mabao kwenye hatua ya nusu fainali ni ule wa 2015/2016, ambao mechi zake za nusu fainali zilikuwa na mabao saba.

Rekodi hiyo nusura ifikiwe katika msimu wa 2019/2020, ambapo mabao sita yalifungwa lakini msimu wa 2016/2017 yalifungwa mabao mawili sawa na ule wa 2020/2021, msimu wa 2017/2018 yalifungwa mabao matano, 2018/19 yakafungwa mabao matatu, ule wa 2021/22 likifungwa bao moja na msimu uliopita yakipachikwa mabao manne.

Ushindi kwa Yanga Jumapili utaifanya kuboresha rekodi ya kuwa timu iliyotinga mara nyingi zaidi hatua ya fainali ya mashindano hayo tangu yalipoanza msimu wa 2015/2016 ambapo hadi sasa inaongoza kwa kufika fainali mara nne.

Kama Yanga itakwama mbele ya Ihefu kesho, Azam inaweza kuungana nayo kama timu iliyotinga fainali mara nyingi ikiwa itaifunga Coastal Union kwani nayo itatimiza fainali nne za mashindano hayo.

Rekodi ya nne inayosakwa ni kwa Ihefu kutinga hatua ya fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza kwani haijawahi kufanya hivyo tangu ianzishwe.

Coastal Union yenyewe ikiwa itaibuka na ushindi dhidi ya Azam FC leo, itaandika rekodi yake yenyewe ya kucheza hatua hiyo kwa mara mbili tofauti kwani tayari ilishafanya hivyo mara moja ambapo ilikuwa ni msimu wa 2021/2022.

Kiungo Jonas Mkude na mabeki Dickson Job na Kibwana Shomary kama Yanga itaingia fainali, wataweka rekodi ya kuwa wachezaji waliowahi kushiriki mechi nyingi za fainali za mashindano hayo ambapo hadi sasa wamefanya hivyo mara nne.

Hapana shaka mechi inayoweza kuwa na ushindani na mvuto wa hali ya juu ni ile ya Azam dhidi ya Coastal Union ambayo mbali na shabaha ya kuingia fainali, kingine kinachoweza kuinogesha ni hamu ya kulipa kisasi ambayo kila upande utakuwa nayo dhidi ya mwingine.

Coastal Union yenyewe inaingia ikiwa inataka kulipa kisasi cha unyonge ambao imekuwa nao kwenye Ligi Kuu msimu huu ambapo katika mechi mbili zilizokutana, imefungwa mchezo mmoja na kutoka sare moja.

Azam FC bila shaka itakuwa na hamu ya kulipa kisasi ya kile ilichofanywa na Coastal Union msimu wa 2021/2022, ilipofungwa mechi ya nusu fainali kwa mikwaju ya penalti 6-5 baada ya timu hizo kutoka sare tasa katika muda wa kawaida wa mchezo.

Katika mchezo wa leo, Azam FC hapana shaka itakuwa inamtegemea zaidi mshambuliaji wake Iddi Selemani 'Nado' ambaye katika mashindano hayo msimu huu amepachika mabao mawili wakati Coastal Union yenyewe matumaini yake yatakuwa kwa Dennis Modzaka aliye na bao moja ambaye ndiye alifunga bao la ushindi katika mechi ya robo fainali.

Yanga yenyewe itakuwa na matumaini makubwa kwa Clement Mzize ambaye ni kinara wa ufungaji kwenye mashindano hayo akiwa amefunga mabao matano akitaka kuvuka rekodi yake ya msimu uliopita huku Ihefu yenyewe ikiwa inasubiria miguu ya kiungo mshambuliaji Marouf Tchakei mwenye mabao mawili kuibeba katika mechi ya leo.

Kocha wa Coastal Union, David Ouma amesema kuwa wanafahamu wanakabiliwa na mechi ngumu lakini watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.

“Mimi kama kocha nina uelewa naamini nitafanya kazi nzuri ni mtihani mzuri kwetu dhidi ya Azam ambayo iko kwenye fomu ina wachezaji wazuri wana Feisal Salum ambaye anawania ufungaji bora ni tishio kwetu, mimi pia nina kipa mzuri (Lay Matampi) mpaka sasa ni sare lakini huenda mechi ikaamuliwa na mchezaji mmoja mmoja.

“Tutakuja na mpango mzuri kwa kuchagua wachezaji ambao wako fiti na wana morali nzuri ya kucheza mchezo huo, kesho (leo) ningependa wachezaji wangu wajitolee wafurahie mpira wapambane ninafahamu Azam ni timu ya namna gani nitapambana kupata mbinu bora zaidi itakayotufanye tupate ushindi,” alisema Ouma

Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry, amesema Coastal Union wanacheza vizuri mpira wa kuzuia hivyo mastaa wake wanapaswa kuwa makini wakati wote, huku beki, Nathaniel Chilambo akisema, wanafahamu hawajafanya vizuri kwenye mashindano yoyote msimu huu, hivyo mchezo wa kesho ni muhimu kwao na unawapa hamasa ya kushinda na kwenda fainali.

Chanzo: Mwanaspoti