Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi hizi zimeshindwa kuvunjwa Ligi Kuu

Kagere 902.png Meddie Kagere

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara imemalizika wiki iliyopita kwa mechi za raundi ya 30 zilipopigwa na kushuhudiwa Yanga ikikabidhiwa taji kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya baada ya kumalizana na Tanzania Prisons, huku Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zikipishana na JKT Tanzania na Kitayosce zilizopanda.

Ruvu na Polisi zimeshuka daraja na kuziachia nafasi JKT na Kitayosce zilizopanda daraja kutoka Ligi ya Championship na timu ya mwisho ya kukamilisha idadi ya timu tatu kutoka daraja hilo itategemea mechi za play-off kati ya zilizomaliza nafasi ya 13 na 14 katika Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa Kigoma.

Mashujaa ilipata nafasi hiyo baada ya kuizidi ujanja Pamba ya Mwanza kwenye mechi za play-off ya Ligi ya Championship, mechi zitakazopigwa wiki ijayo kukamilisha msimu wa 2022-2023.

Lakini wakati ligi ikifikia tamati na klabu kwenda mapumziko ya muda mfupi kisha kufanya usajili kupitia dirisha dogo kabla ya kurejea kuanza vita mpya ya 2023-2024, kuna baadhi ya rekodi zimeendelea kuwatesa mastaa wa kigeni na wazawa katika ligi hiyo iliyojiandaa kuingia msimu wa 60.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya rekodi hizo zilizoshindwa kudumu na kuendelea kusubiri labda kwa msimu ujao kama mastaa wa timu zote watarudi na nguvu mpya za kupindua meza kibabe.

HAT TRICK YA WATANI

Licha ya Simba na Yanga na kukutana kwenye Ligi ya Bara kwa miaka 58 tangu ligi hiyo ilipoasisiwa rasmi 1965, imeshuhudiwa hat trick moja tu ilipopigwa kwenye pambano lililobaki la kusisimua hadi leo lililochezwa Jumanne ya Julai 19, 1977.

Katika pambano hilo, Yanga ilipigwa mabao 6-0 na Simba iliyokuwa inalipa kisasi cha mwaka 1968 walipofumuliwa mabao 5-0 kwenye mechi iliyopigwa Juni Mosi, ambapo Abdallah 'King' Kibadeni alifunga hat trick ambayo haijawahi kujibiwa na mchezaji yeyote hadi leo hii.

Licha ya kushuhudiwa mechi kadhaa za watani zikizalisha mabao mengi ikiwamo sate ya 4-4 kwenye mchezo uliopigwa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha mwaka 1996 na kipigo cha 5-0 ilichopewa tena Yanga katika mchezo uliopigwa Mei 6, 2012 hakuna mchezaji aliyeweka kufunga tena hat trick.

Hata msimu huu, baadhi ya mashabiki waliviangalia vikosi vya timu zote mbili na aina ya wachezaji iliyonayo, wakabeti huenda mambo yakawa mambo, lakini mechi ya kwanza baina yao iliisha kwa sare ya 1-1 na ile ya marudiano Yanga ililala 2-0 na rekodi ya Kibadeni ikaendelea kudumu.

REKODI YA MMACHINGA

Pamoja na kushuhudiwa wachezaji wakali wa kigeni na wazawa wakikipiga kwenye Ligi Kuu Bara kwa misimu kadhaa iliyopita, msimu huu kuna wadau waliamini ile rekodi ya mabao mengi katika msimu mmoja iliyowekwa na Mohammed Hussein 'Mmachinga' enzi akiwa Yanga itavunjwa, lakini wapii! Mmachinga aliyekipiga pia Bandari Mtwara, Simba, Mmbanga FC na Twiga Sports, alifunga mabao 26 msimu wa 1998.

Kwa hesabu za haraka ni kwamba hadi sasa ni miaka 25 rekodi hiyo ya Mmachinga imeshindwa kufikiwa, japo msimu wa msimu wa 2006, straika aliyekuwa akikipiga Mtibwa Sugar, Abdallah Juma 'AJ' aliikaribia kwa kufunga jumla ya mabao 25 na tangu hapo hakuna tena aliyewahi kuisogelea rekodi hiyo hadi leo.

Straika huyo wa zamani aliyeichezea Taifa Stars, pia ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 153 katika misimu 13 kuanzia 1993-2005 akifukuziwa kwa karibu na John Bocco aliyefunga mabao 150 katika misimu 14 tangu 2008-2023.

Ni bahati mbaya tu, Bocco licha ya juhudi kubwa ya kutupia mabao akiwa na Azam FC kisha kutua Simba misimu mitano iliyopita na huku jua likiwa linaeleka kuzama, ameshindwa kuifikia huku kukiwa na taarifa huenda mkongwe huyo akabadilishiwa majukumu Msimbazi na hivyo kukwama.

Nani anajua msimu ujao utakuwaje baada ya msimu huu kushuhudiwa rekodi ya Mmachinga ikishindwa kufikiwa kama ilivyokuwa ile ya Kibadeni ya kupiga hat trick kwenye Kariakoo Derby.

MABAO YA KAGERE

Meddie Kagere kwa sasa yupo Singida Big Stars baada ya mwishoni mwa msimu uliopita kutemwa na Simba, lakini wakati anaondoka Msimbazi, nyota kutoka kutoka Rwanda aliweka rekodi tamu kwa mastaa wa kigeni katika Ligi Kuu Bara ambayo hata yeye mwenyewe ameshindwa kuifikia.

Kagere alitua Msimbazi kutoka Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-2019 na kufunga jumla ya mabao 23 akiipiku rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Amissi Tambwe alipokuwa Yanga ya nyota wa kigeni kufunga mabao mengi kwenye msimu mmoja alipotupia 21 na kubeba kiatu 2015-2016.

Msimu wa pili kwa staa huyo, alifunga mabao 22 na kutetea tuzo ya Mfungaji Bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo ya ufungaji mara mbili mfululizo. Simon Msuva akiwa na Yanga na Tambwe kama ilivyo kwa John Bocco ni wachezaji pekee tangu 2000 kuwahi kupata tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu mara mbili kwa misimu tofauti. Bocco alitwaa 2011-2012 enzi akiwa na Azam FC kisha akarudia tena 2020-2021 akiwa na Simba, wakati Tambwe aliinyakua 2013-14 akiwa Simba na kurudia 2015-2016 akiwa na Yanga, ilihali Msuva yeye alibeba 2014-2015 na 2016-2017, mara zote akiwa na Yanga kabla ya kuutwa Difaa El Jadida.

Hivyo, kwa msimu huu tena imeshuhudiwa ligi imeisha huku rekodi hizo alizoziweka MK14 enzi akiwa Msimbazi zikishindwa kufikiwa, licha ya Fiston Mayele, Saido Ntibazonkiza, Kagere mwenyewe na wakali wengine ambao walichuana msimu huu kucheka na nyavu.

MAKIPA KUFUNGA

Juma Kaseja anashikilia rekodi ya kufunga mabao kwenye Ligi Kuu Bara, akiwa na mawili moja akifunga enzi akiwa na Yanga mwaka 2009 wakati wanaizamisha Toto Africans kwa mabao 2-1, kisha kurudia tena 2011-2012 wakati akiizamisha Simba ikiizamisha Yanga kwa mabao 5-0.

Kwa msimu huu imeshuhudiwa tu makipa wakijifunga mabao na kuzinufaisha timu pinzani kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini hakuna kipa aliyejaribu kuipita rekodi ya Kaseja ya kuibeba timu yake kwa kufunga kwenye Ligi Kuu Bara.

Makipa Faruk Shikhalo aliyekuwa Mtibwa Sugar na Yona Amosi wa Tanzania Prisons walijifunga msimu huu kama ilivyowahi kuwakuta Hussein Masalanga na Mohammed Yusuf wote wakiwa makipa wa Dodoma Jiji.

Ally Yusuf 'Barthez' aliwahi pia kufunga kwenye Ligi Kuu mwaka 2016 wakati Yanga ikitoka sare ya 2-2 na Majimaji, huku Idd Pazi 'Father' akifanya hivyo kwenye Kariakoo Derby mwaka 1985 kabla ya Kaseja kumjibu 2012 na rekodi zao zimeendelea kudumu pengine kwa ugumu wa makipa kwafunga wenzao, labda iwe kwa penalti au itokee tu kama zali tu. Tusubiri msimu ujao tuone inakuwaje?

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: